Wednesday, May 8, 2013

TGNP Waadhimisha Siku ya Wanawake Duniani


oxoxox e4b07
TGNP kwa kushirikiana na wanaharakati wa masuala ya haki  na usawa wa Kijinsia, haki za Binadamu, Demokrasia, Utawala bora na Maendeleo  wameungana na wanaharakati wengine duniani katika kusherehekea na kutafakari maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ili kuwezesha jamii kutambua mchango wa wanawake  kisiasa, kijamii na kiuchumi na matokeo ya harakati zao, changamoto zinazowakabili wanawake na kuendelea kutafakari mbinu za kuboresha kwa kipindi cha baadae.


Kauli mbiu ya kimataifa mwaka huu ni “Uelewa wa Masuala ya Jinsia katika Jamii: ongeza Kasi” Ukosefu wa uelewa wa masuala ya Kijinsia ni kikwazo kikubwa cha kupambana na tatizo la ukatili wa Kijinsia katika ngazi ya jamii hadi kitaifa, kuna changamoto kubwa ya kukosekana kwa uelewa mpana wa dhana ya usawa na haki za kijinsia ambayo imesababisha hata mgawanyo wa rasilimali katika maeneo mbalimbali kutokuzingatia hali halisi na mahitaji ya Kijinsia, mfano uandaaji wa bajeti za kiserikali, ujenzi wa miundombinu, utoaji wa huduma za kijamii kama maji, afya, chakula nk.


TGNP na wanaharakati wengine tunatumia fursa hii ya leo, kupaaza sauti zetu kudai haki ya kuangalia suala la usawa wa kijinsia, wanawake wanapate haki zao za msingi hasa katika suala la matibabu, uzazi salama, elimu, maji salama, ushiriki wa kutosha katika nafasi za ajira ngazi zote na ushiriki sawa katika nafasi za maamuzi na ulinzi wa kutosha kutokana na kukithiri kwa ukatili wa Kijinsia.


Ndio maana leo kwa kushirikiana na wanaharakati ngazi ya jamii na GDSS, tunazindua Ilani ya Haki za wanawake katika katiba mpya na tukiongozwa na kauli mbiu yetu ya “Ajenda ya haki  na usawa wa Kijinsia  katika Katiba mpya”


TGNP tumetambua kuwa uelewa wa masual ya Kijinsia ni pamoja na kuyaingiza kwenye Katiba mpya kama sheria mama ya nchi, kuweka mikakati ya kuingiza masuala ya wanawake katika sera, mipango na bajeti kila mwaka.

Mchakato wa TGNP  wa Madai ya Katiba Mpya umetokana na ushiriki mkubwa wa wadau mbalimbali wa Mtandao wa Jinsia. Kwanza kabisa ni wadau wa mikutano ya kila Jumatano (GDSS) inayofanyika [hapa]katika viwanja vya TGNP. Mikutano hii kuanzia tarehe 14/03/2012, hadi tarehe 17/10/12 ilikuwa ikijadili suala zima la katiba mpya na kutoa mapendekezo yaliyoainishwa katika Ilani hii inayozinduliwa leo. Vile vile TGNP ilishiriki katika Kongamano lililoandaliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) lilohusisha wanawake takribani 110 kutoka taasisi zaidi ya hamsini zilizowakilisha asasi mbalimbali kutoka mikoa 19 ya Tanzania bara na visiwani tangu tarehe 22-24 Oktoba 2012. Kongamano hili lilijadili na kukubaliana mambo ya msingi ya madai ya wanawake katika katiba mpya.


Kwa kifupi tunaamini kwamba madai haya yametokana na sauti mbalimbali za wadau wanaotetea haki za wanawake na hususani haki za kikatiba na tunaamini yatafanyiwa kazi. Madai ya sasa hivi ya mwafaka mpya wa kitaifa unatokana na mwendelezo wa harakati za raia na hususani za wanawake za  kutaka mabadiliko ya msingi yatakayowawezesha kukabiliana na changamoto zitokanazo na mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchumi wa dunia, mapinduzi ya  teknologia ya mawasiliano, na kuimarika kwa mifumo kandamizi inayoashiria kumbebesha raia maskini na hasa mwanamke mzigo mkubwa zaidi  kutokana na changamoto za mabadiliko haya.                         

                                        
Kwa mfano msukosuko wa kiuchumi uliokumba nchi za kibepari tangu mwaka 2008, umezifanya nchi hizi chini ya uongozi wa matajiri wachache wa dunia, kujizatiti zaidi katika kupora rasilimali za nchi zetu wakishirikiana na viongozi wachache na mabepari uchwara wa nchi zetu wakiwa wanaume na hata wanawake wachache.
 
Tunataka katiba iliyotokana na mchakato uliyoshirikisha sauti za wanawake na wanaume, na iliyoweka bayana makubaliano ya misingi mikuu itakayoongoza nchi yetu. Vilevile tunataka katiba iliyojengewa misingi ya usawa, utu na inayokataza aina zozote za ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia.

Pamoja na madai 18 yaliyoainishwa kwenye madai yetu, Sisi wanaharakati tumeweka mikakati kuhakikisha Sauti na madai yetu yanaingizwa katika Katiba mpya. Tukihamasishana:- kukubaliana kuhusu misingi mikuu ( kuwa na uelewa wa pamoja na sauti moja), ushiriki kwenye mikutano ya tume, Kushiriki kikamilifu kwenye mabaraza ya katiba ya kata na wilaya, kudai usawa katika uundaji wa bunge la katiba, ushiriki katika kura za maoni, kutumia njia zilizowekwa za kufikisha ujumbe kwa tume, kuhamasisha wanawake washiriki kila hatua ya mchakato.

No comments:

Post a Comment