Mshindi wa mbio za mwaka 2012 za
Boston Marathon, Wesley Korir, aliyemaliza wa tano mwaka huu, ameambia
BBC kuhusu hofu yake pindi aliposikia milipuko miwili iliyotokea Boston
Marekani.
Milipuko hiyo ilitokea karibu na msitari wa
mwisho wa kumalizia mbio hizo na kuwajeruhi takriban watu 140 takriban
saa mbili baada ya mshindi kumaliza mbio hizo.
Alikuwa akisherehekea ushindi wa mkenya Rita Jeptoo katika mbio za wanawake.
"furaha yetu ni kuwa tulikuwa tayari tumeondoka katika eneo hilo,'' Korir aliambia BBC.
Bi Jeptoo anatoka katika eneo bunge la Cherangany, ambalo bwana Korir ni mbunge wake baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika mwezi jana.
Licha ya milipuko hiyo pamoja na jukumu lake la kisiasa, Korir amesema kuwa ataendelea kushindana katika mbio za marathon hata ikiwa Boston itaandaa mbio zengine mwaka ujao.
Alisema kuwa punde tu baada ya kusikia habari hiyo aliwapigia simu wakwe zake kuwajulia hali kwani walikuwa wamemtembelea pamoja na kocha wake.
Balozi wa Kenya nchini Marekani amesema kuwa hana taarifa zozote kuhusu wakenya waliojeruhiwa kwenye mashambulizi hayo.
Raia wawili wa Afrika Kusini walitibiwa baada ya kupata majeraha
Lelisa Desisa, wa Ethiopia alishinda mbio za wanaume mbele ya mshindani wake Micah Kogo.
Mbio hizo mwaka huu zilikuwa na wanariadha 23,000 na zilitazamwa na mamia ya mashabiki.
No comments:
Post a Comment