Thursday, April 11, 2013
JELA MIAKA 20 KWA KUKUTWA NA NYAMA YA TEMBO
MAHAKAMA ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, imemhukumu mkazi wa kijiji cha Kisisha Wilaya ya Siha Simon Elias (47), kutumikia kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya Shilingi milioni 15 baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili ikiwemo kukutwa nyara ya serikali aina nyama ya tembo kilo 7 yenye thamani milioni 1.5 kinyume na sheria.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Hai Martha Mahumbuga mbele ya mwendesha mashitaka wa polisi wa mahakama hiyo Roymax Membe alisema ametoa hukumu hiyo baada ya kuridhika na ushaidi uliotolewa na upande wa mashitaka.
Awali hakimu huyo alidai kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo mnamo Machi 27 mwaka 2010 majira ya saa kumi usiku wakati mtuhumiwa alipokamatwa na bunduki aina rifle kinyume na sheria ya udhibiti wa silaha kifungu cha 4 (1) na 34 (2) sura ya 223 ya mwaka 2002.
Alisema mtuhumiwa alitenda kosa la pili la kukutwa na nyara ya serikali, nyama ya tembo kilo 7 yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 1.5 kinyume na taratibu za nchi za uhujumu wa uchumi kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1984.
Mwendesha mashitaka aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kutokana na mtuhumiwa kumiliki silaha kinyume na taratibu kulikochangia zaidi ujangili na kusababisha jeshi la polisi kutumia nguvu kubwa kukabiliana na uhalifu.
Awali mtuhumiwa huyo alipopewa nafasi ya kujitetea aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu hiyo kutokana na kutegemewa na familia.
Hakimu mfawidhi alikubali ombi la Mwendesha mashitaka na kumuhukumu mtuhumiwa huyo kutumikia ili adhabu hiyo iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hizo.
Mwandishi: BAHATI CHUME
Mhariri: JOHNSON JABIR
Source: http://www.wavuti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment