Tuesday, April 16, 2013

DAWA ZA MSD KUWEKEWA ALAMA MAALUM

Ili kuondoa malalamiko yanayotupwa Serikalini kutokana na vitendo vya baadhi ya watumishi wasio waaminifu, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani amesema Serikali sasa imeamua kuweka alama maalumu katika dawa ambazo watakuwa wakizisambaza kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali zote nchini kuepusha ubadhirifu ambao hufanywa na watumishi wasio waaminifu wa Idara ya Afya.

Alama hiyo itakuwepo pia kwenye vidonge na itasaidia kuondoa ubadhirifu huo na vituo vya afya kuwepo na dawa wakati wote.

“Uamuzi huo umefikiwa baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ya kukosa dawa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitalini baada ya kutibiwa na kuambiwa wakanunue katika maduka ya dawa,” alisema.

Alisema tofauti na kulinda dawa hizo pia alama hizo zitawarahisishia kazi wakaguzi kwa kugundua uhalifu huo pindi dawa hizo zitakapokutwa katika maduka ya watu binafsi ya kuuzia dawa.

“Tofauti na hayo pia alama hizo zitasaidia kutokuingia kwa dawa dhaifu sokoni ambazo zinadhoofisha afya ya mlaji kwa kuyatia magonjwa usugu,”alisema Mwaifwani.

Alisema ni jukumu la wananchi kuwa wazalendo na nchi yao kwa kuhakikisha dawa zinazosambazwa na MSD zinatumika kwa walengwa.

Mwaifwani aliyasema hayo wakati wa semina ya siku moja ya kuhamasisha watendaji wa sekta ya afya juu ya mpango mpya wa usambazaji wa dawa iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

via HabariLeo


No comments:

Post a Comment