Friday, February 8, 2013

UKATILI WA KIJINSIA WACHANGIWA NA KUTOKUJUA SHERIA

mkuru

CHAMA cha wandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) kimebaini kuwa kuongezeka kwa kesi za ukatili wa kijinsia kumechangiwa na kutojua sheria na kutokuwepo kwa mifumo madhubuti ya kuripoti ikiwa ni pamoja na jamii kutobadilishana mawazo.
Akiwasilisha ripoti ya utafiti huo Dar es salaam jana Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valerie Msoka alisema hayo yamebainika wakati wa utafiti wa awali uliofanywa na mashirika ya kutetea haki za binadamu ambayo ni Chama cha wanasheria wanawake (TAWLA), Chama cha wanasheria wanawake Zanzibar(ZAFELA), Kituo cha usuluhishi (CRC), Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) pamoja na Tamwa bara na Zanzibar.
Alisema kuwa utafiti huo umebaini kuwa asilimia 17 tu ya wananchi ndiyo wenyeuelewa wa sheria za ukatili hali inayochangia jamii kutofatilia haki zake pindi zinapovunjwa ambapo na wakati mwingine kutokuripoti kabisa kesi hizo.
“Tumebaini kuwa Lindi vijijini ndiyo inayoongoza kwa kuwa na uelewa mdogo wa asilimia 12 ya wakazi ukilinganisha na asilimia 21 ya uelewa kwa Wilaya zote kwa mfano Ofisa wa Polisi wa Wilaya ya Lindi alisema kesi nyingi huripotiwa katika hatua ya familia na hufikishwa mahakamani baada ya kushindwa kupata suluhu na hivyo kuwa katika hatari ya kupata haki” alisema Msoka.
Alibainisha kuwa hali ya kutokuwa na mfumo maalum wa kuripoti kunaweka mazingira ya kutokupatikana kwa haki ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa takwimu sahihi ya kesi za ukatili.
Msoka alizitaja Wilaya zilizohusika katika utafiti huo kuwa ni Wete(Pemba kaskazini), Magharibi (Unguja), Kusini Unguja(Kusini Unguja), Kisalawe (Pwani) Newala (Mtwala), Lindi vijijini(Lindi), Mvomero (Morogoro) na Wilaya za Kinondoni na Ilala, Dar es Salaam.
Alisema kwa pamoja mashirika hayo yatatekeleza mpango wa usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake(GAWE) ambao unafanywa kwa ushirikiano na Serikali ya Denmark.

No comments:

Post a Comment