Katika kile kinachoonekana kutilia
mkazo agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Emanuel Nchimbi alilolitoa
hivi karibuni la kuwataka watu wanaomiliki silaha isivyo halali
kuzisalimisha, kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha,
Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas alitoa msisitizo kwa watu wa
aina hiyo waliopo mkoa wa Arusha kwamba, ni nafasi yao sasa kujitokeza
na kusalimisha silaha hizo bila kuchukuliwa hatua kwani wamepewa muda wa
mwezi mmoja.
Kamanda Sabas aliyasema hayo jana
ofisini kwake wakati akizungumza na waaandishi wa habari, na kufafanua
kwamba,nafasi hiyo ya usalimishaji wa silaha hizo imeanza toka tarehe 4
mwezi huu na milango itafungwa rasmi tarehe kama hiyo mwezi ujao
mwakani.
Aliwataka watu hao waliopo ndani
ya mkoa huu wajitokeze na kusalimisha silaha hizo kwani hawatachukuliwa
hatua ndani ya siku hizo ila baada ya tarehe hiyo kupita, Jeshi la
Polisi mkoa wa Arusha litafanya msako mkali na yeyote atakayekamatwa
atakuwa ni mhalifu kama wahalifu wengine wa aina hiyo.
Akitoa onyo katika kipindi cha
kuelekea mwisho wa mwaka , Kamanda Sabas alisema kwamba mara nyingi uwa
kunakuwa na makundi ya watu wanaojiingiza katika kufanya matukio ya
uhalifu kwa madai ya kujiongezea kipato, hivyo amewataka watu hao kuacha
mara moja tabia hiyo kwani jeshi la polisi mkoa wa Arusha limejipanga
vyema kukabiliana nao.
Kwa upande wa Usalama barabarani
aliwataka watumiaji wa vyombo vya usafiri na watembea kwa miguu kuwa
makini katika matumizi ya barabara na kutakiwa kuzingatia sheria za
usalama barabarani. Alisema wananchi waondoe dhana ambazo si sahihi
kwamba, mwisho wa mwaka lazima zitokee ajali nyingi bali hayo
yanasababishwa na madereva na watembea kwa miguu kutozingatia sheria za
usalama barabarani.
Mwisho Kamanda Sabas, aliwaomba
wananchi wa mkoa wa Arusha waendelee kushirikiana na jeshi la polisi
katika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwani bila hivyo suala la
kutokomeza uhalifu litakuwa ni ndoto.
No comments:
Post a Comment