Friday, November 9, 2012

WIZARA YA ELIMU YAINGILIA KATI SHULE KUFUNGIWA BAGAMOYO

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeingilia kati mgogoro ulioibuka katika Shule ya Sekondari ya Bagamoyo kwa kuagiza viongozi wa Idara ya Elimu ya Wilaya ya Bagamoyo kupeleka ripoti kuhusu chimbuko la migogoro hiyo ili wizara iweze kuchukua hatua haraka.

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi, Phillipo Mulugo, alisema baada ya wizara yake kupata taarifa za mgogoro imechukua hatua ya kumwagiza Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Bagamoyo kupeleka taarifa za chanzo ili hatua zichukuliwe haraka.



Jumatatu wiki hii Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, alitangaza kuifunga shule hiyo kwa kipindi kisichojulikana kutokana na mgogoro wa kidini katika shule hiyo ambao upelekea amani kutoweka.

Mahiza alisema amechukua uamuzi huo ili kuiwezesha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutafuta ufumbuzi wa migogoro, utoro wa walimu na kudumisha amani katika shule hiyo, “Baada ya kufika nimebaini bado kuna tatizo, kwani hadi nafika jana (juzi) nimekuta wanafunzi 356 kati ya 740 walioandikishwa katika shule hiyo hawajulikani walipo na Mkuu wa Shule hajui walipo,” alisema Mahiza.

Hata hivyo, taarifa ambazo NIPASHE ilizipata toka shule hapo zinaeleza kuwa kufungwa kwa shule hiyo kulifuatia wanafunzi tisa kuandikiwa barua ya kusimamishwa masomo, maamuzi ambayo yaliamriwa na Bodi ya Shule hiyo, lakini wanafunzi hao walikataa kuzipokea barua hizo.

Baada ya wanafunzi hao kukataa kuzipokea barua hizo, kulizuka vurugu za wanafunzi shule hapo ambao walikuwa wakiwaunga mkono wanafunzi walioandikiwa barua hizo na hivyo serikali ya mkoa kuchukua hatua ya kuifunga shule kwa muda usiojulikana.

---
via NIPASHE


No comments:

Post a Comment