SERIKALI imeamua kuagiza dawa zote za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI (ARVs) kutoka India, baada ya Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI) kudaiwa kuzalisha dawa feki.
Aidha, imepanga kutoa tamko lake rasmi bungeni keshokutwa kuhusu sakata hilo la dawa feki za ARVs ambapo watumishi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), walioongezeka katika kusimamishwa kazi watatajwa.
Katika tamko lake, Serikali kupitia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, itabainisha hatua ilizochukua na inazoendelea kuzichukua kuhusu wote waliohusika katika sakata hilo lililotikisa nchi.
Hilo limefahamika baada ya Kamati ya Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya kikao chao juzi jioni katika Ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni mjini hapa, na suala hilo liliibuka katika mjadala.
Chanzo chetu (HabariLeo) kilibainisha kuwa katika tamko hilo, pia kutaelezwa aina za dawa zitakazotumika kwa wenye Virusi Vya UKIMWI, ikiwa ni hatua ya kufidiwa zile zilizoondolewa baada ya kubainika kuwa feki.
Habari hizo zilisema kuwa Wabunge walielezwa kuwa dawa hizo kwa hivi sasa zinaendelea kuagizwa kutoka India wakati TPI kinachodaiwa kutengeneza dawa hizo kikiwa kimefungiwa.
Awali sehemu ya dawa hizo zilikuwa zikiagizwa kutoka India na Serikali na nyingine zilikuwa zikitoka katika kiwanda hicho chenye makao yake makuu jijini Arusha. Jumla ya wagonjwa 500,000 wanapata dawa hizo. Dawa hizo zinazoagizwa na Serikali zinalipwa na Taasisi ya Global Fund.
“Tulielezwa kuwa dawa hizo sasa zote zinaagizwa kutoka India na hatua hiyo ilichukuliwa mara moja tu baada ya kiwanda kile kinachodaiwa kutengeneza dawa feki kusimamishwa kuzalisha dawa hizo,” kilieleza chanzo chetu ndani ya kikao hicho cha wabunge wa CCM.
“Katika kikao tumeelezwa kuwa watumishi wa MSD waliosimamishwa kazi imeongezeka na tamko la Serikali litakatolewa Jumatatu litaeleza zaidi kiundani,” aliongeza mtoa habari wetu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, suala hilo liliibua hisia kubwa kutoka kwa wabunge, lakini baadaye walitulizwa na maelezo ya Serikali kuhusu jinsi walivyoelezea hatua zilizochukuliwa kutokana na sakata hilo. Katika kuoneshwa kukerwa wabunge, walitaka watumishi wa MSD washitakiwe na kufukuzwa kutokana na uzembe huo waliouonesha.
Hatua ambazo tayari Serikali imeshazichukua hadi sasa ni kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Joseph Mgaya kutokana na kubainika kuwapo na kusambaa kwa ARVs.
Mbali na Mkurugenzi huyo, pia imemsimamisha Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora, Daud Maselo na Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora wa Dawa, Sadick Materu. Dawa hizo bandia zilibainika mwanzoni mwa Septemba mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime baada ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kufanya ukaguzi.
Dawa hiyo yenye jina la biashara TT-VR 30 toleo namba OC.01.85, iligundulika kuwa ni bandia baada ya kuifanyia uchunguzi wa kimaabara.
Baada ya kubaini tatizo hilo, walifanya ukaguzi kati ya Agosti 6 hadi 31, mwaka huu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara na mikoa mingine nchini na kubainika nyaraka zinaonesha kuwa TPI iliiuzia MSD dawa hiyo. Tayari kiwanda hicho kimesitishwa kutengeneza na kusambaza dawa hizo.
Awali makopo 9,570 ya dawa hiyo yalirejeshwa, MSD walikuwa wakiendelea na utaratibu wa kuyakusanya makopo mengine 2,600.
Dawa hiyo ilitengenezwa Machi mwaka huu na muda wa matumizi yake unatarajiwa kuwa Februari mwakani huku zikiwa na rangi mbili tofauti, njano na nyeupe.
Dawa zilizokuwa na rangi ya njano zilikuwa na kiambata cha Efavirenz badala ya viambata aina ya Niverapine, Lamivudine na Stavudine vilivyopaswa kuwepo.
Vidonge vilivyokutwa kwenye vifungashio vya dawa husika vilikuwa tofauti na vifungashio vilivyosajiliwa na TFDA.
Akizungumza na gazeti hili (HabariLeo) jana katika Viwanja vya Bunge, Waziri Mwinyi alikiri kuwa keshokutwa atatoa tamko la Serikali bungeni, lakini akakataa kuzungumzia kiundani juu ya tamko hilo.
“Siwezi kukuambia sasa hivi nitakachozungumza kwani itakuwa haina maana subirini tu kauli ya Serikali mtasikia yote unayotaka kujua,” alisema Dkt. Mwinyi.