Monday, November 5, 2012

MWANAFUNZI UTALII ACHOMWA KISU KISA WIVU WA MAPENZI

Habari hii imeandikwa na Pascal Michael, Musoma, na imeshirikishwa kwetu na Magiri Paul wa wotepamoja.com

Mwanachuo wa Musoma Utalii aitwaye Rose Kanyambo  (21), alishambuliwa kwa visu mgongoni na ubavuni na mtu anayedaiwa  kuwa ni mpenzi wake ambaye pia ni mwanachuo, baada ya kukataliwa kuendeleza urafiki.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Mara, Irege Ngaregeza ametibitisha kumpokea mgonjwa huyo siku ya Ijumaa, Novemba 2, mwaka huu ambapo binti huyo alikuwa na jeraha la kuchomwa kisu mgongoni na ubavuni alifika hospitali hapo katika hali mbaya lakini juhudi za madaktari za kuokoa maisha yake zilifanikisha hali yake kuimarika.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa taabu wodini, Rose alisema kuwa siku ya Ijumaa majira ya saa mbili asubuhi akiwa chuoni maeneo ya Kamunyonge katika Manispaa ya Musoma, ghafla kijana aitwaye John Ogolla alitokea  chuoni hapo na kuanza kumshambulia kwa kumchoma kisu mgongoni mara mbili  na ubavuni na kutokwa na damu nyingi.

Rose anasema alifanikiwa kukimbia hadi alipokuwa anaishi, umbali mchache kutoka chuoni na kisha kudondoka chini baada ya nguvu kumuishia. Anasema majirani walipomsaidia na kufanya jitihada za kumpeleka hospitalini.

Binti huyo alieleza chanzo cha kuchomwa kisu ni kumkataa kijana huyo kuhusiana na uhusiano wa kimapenzi. Kijana huyo amekuwa akimlazimisha mara kwa mara kuwa na uhusiano wa kimapenzi lakini yeye hakutana na ndipo alipomjeruhi.

Hata hivyo, baadhi ya majirani na wanachuo  walisema kuwa  Rose na John walikuwa na mahusiano ya muda mrefu na kijana huyo amekuwa akimsaidia  mambo mengi sana lakini ghafla mpenzi huyo alibadilika na kumkataa bila sababu za msingi.

Inasemekana Ogolla baada ya kutekeleza tukio hilo, “alikuwa ameandaa barua ambayo aliandika ya ama kufa yeye au Rose Kanyambo na pia alichukua picha ambayo walipiga pamoja na kuichora alama ya X kwa kutumia marker pen” alisema shuhuda mmoja.

Jeshi la polisi linamshikilia John Ogolla kuhusiana na tukio mara baada ya upelelezi kukamilika atapandishwa kizimbani.