Sunday, November 4, 2012

MSAKO KUANZA KWA WALE WANAOTUMIA NAMBA BINAFSI KWENYE MAGARI YA SERIKALI

SERIKALI imesema zimebaki  siku 11 kabla ya kuanza kuwakamata watumishi wote wanaotumia namba za kiraia kwenye magari yake,kinyume cha sheria na utaratibuAkizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Injinia John Ndunguru, alisema serikali iliweka utaratibu unaozuia matumizi ya namba za kiraia kwenye magari yake isipokuwa kwa kibali maalum kutokana na kubaini kuwa, kupitia namba hizo, magari ya Umma yalikuwa yakitumiwa vibaya na baadhi kupotea.
Alisema Oktoba 19 mwaka huu waziri wa wizara hiyo, John Magufuli alitoa agizo kuwa hadi Novemba 15 mwaka huu itakuwa  siku ya mwisho ya kusajiliwa magari yote ya Umma kulingana na sheria na taratibu za nchi.
Akifafanua, Ndunguru alisema magari yote ya Umma katika wizara, Idara za serikali na taasisi za Umma yanayotumia nambaza kiraia, magari hayo yanapaswa kusajiliwa kwa utaratibu uliowekwa na Serikali ambao unataka magari yote ya Umma kuwa na namba zifuatazo, magari ya Serikali Kuu yatakuwa na mamba za ST, Serikali za Mitaa namba za SM, Mashirika ya Umma namba za SU na yale yaliyotolewa na Washirika wa Maendeleo kwa ajili ya miradi wanayoisaidia, namba za DFP.
Mengine ni yale ya vyombo maalum kama Jeshi (JW), Polisi (PT), na Magereza ambao wataanza kutumia namba mpya za MT.
Ndunguru alisema baada ya agizo serikali itaendesha msakao mkali wa kukamata magari ambayo yatakuwa bado hayajasajiliwa kwa namba za serikali.
   
 “Sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 kifungu Na. 30 na iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004 inaipa wizara ya ujenzi kusajili na kutunza kumbukumbu za magari yote ya Serikali ambayo yatapewa namba zitakazotanguliwa na JW, PT, ST (sheria na 62), na DFP (GN. No.517 ya Novemba 29, 2002”alifafanua Ndunguru.
Ndunguru aliwatahadharisha wote ambao wana magari ya Umma, ambayo bado yanatumia namba za kiraia kubadili usajili huo, haraka ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa kufikishwa mahakani kwa makosa ya jinai.