Hatimaye ile ahadi ya Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe
kuhusiana na kuanzishwa kwa usafiri wa daladala za treni jijini Dar es
Salaam utakaoanza Oktoba mwaka huu, imeanza kutekelezwa jana asubuhi na
wananchi mbalimbali wakanufaika na huduma hiyo kwa usafiri kati ya
Ubungo Maziwa na Posta, Stesheni kwa reli ya TRL.
Usafiri mwingine wa treni utapitia reli ya TAZARA kutoka Kurasini hadi Mwakanga. Treni
hiyo iliyokuwa na mabehewa sita likiwemo moja lililotengwa maalumu kwa
ajili ya wanafunzi, ilionekana kufurahiwa na wananchi waliokuwa
wamepanda kutokana na utulivu uliokuwamo ndani yake huku ukisindikizwa
na burudani za muziki na matangazo kutoka kwa wahudumu waliokuwemo ndani
ya kila behewa huku ikipokewa kwa shangwe katika maeneo yote ilipopita
kwa wananchi kuwapungia mikono abiria waliokuwa ndani.
Ndani ya treni hizo pia kulikuwa na usalama wa kutosha kutokana na kuwapo askari wengi ndani ya treni na vituoni kuanzia.
Akizungumza
wakati wa kuzindua rasmi safari hizo leo, Waziri Mwakyembe aliwataka
wananchi watakaokuwa wakitumia usafiri huo kuvumilia kasoro mbalimbali
zitakazojitokeza katika siku za mwanzo na kuahidi kwamba serikali
itaendelea kuboresha huduma hizo kila uchao.
Dkt. Mwakyembe
aliwataka wakazi wa Dar es Salaam, hasa kwenye maeneo yaliyo karibu na
reli kutunza miundombinu ya usafiri huo, ikiwa ni pamoja na kukomesha
tabia ya baadhi ya watu kugeuza maeneo ya njia za reli kuwa majalala ya
kutupia uchafu.
Akawataka viongozi wa serikali za mitaa ambako
reli zinapita waongoze uangalifu ili usafiri huo uendelee vyema na
kuwapunguzia adha ya usafiri na foleni wakazi.
“Nawaombeni
Watanzania tuunge mkono usafiri huu, kwanza mzuri, wa haraka na pia wa
kistaarabu, mtu unaweza kufunga tai yako kuanzia mwanzo hadi mwisho wa
safari na isitingishike, tuachane na maneno ya watu wasioutakia mema
usafiri huu...” “...Inasikitisha kuona kuwa katika baadhi ya maeneo,
reli zimegeuzwa kuwa dampo na kujaa uchafu... nawaomba tujitahidi
kutunza maeneo haya ya miundombinu ya reli," alisema Dk Mwakyembe huku
akishangiliwa na wananchi.
Alisema usafiri huo utakaoendeshwa na
Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) na Shirika la Reli
Tanzania (TRL), utakuwa ukianza saa 11.00 alfajiri hadi saa 2.00 usiku.
Treni zitakuwa
zikipumzika kuanzia saa 5.00 asubuhi hadi saa 9.00 alasiri na kupumzika
katika siku za Jumapili na sikukuu. Nauli ni Sh 400 kwa mtu mzima kwa
TRL na Sh 500 kwa ile ya Tazara wakati nauli kwa mwanafunzi ni Sh 100.
Abiria
David Makalinja aliiomba Serikali kuondoa dosari ya ratiba
ya treni hiyo kwa siku ya jana ili kuwafanya watumiaji wa usafiri huo
kwenda na muda.
Alisema
kama kutakuwa na ratiba rasmi ya kupita kwa treni hiyo katika vituo
vyake, itawasaidia wafanyakazi kujua muda wa kufika kazini, tofauti na
hali iliyojitokeza jana ambapo abiria walilazimika kuisubiri treni hiyo
katika kituo cha Ubungo kwa zaidi ya saa 3 kuanzia saa 12.20 hadi saa
3.30.
Hata hivyo, kwa
mujibu wa Mkurugenzi wa TRL, Amani Kisamfu, tatizo hilo limesababishwa
na hitilafu ndogo ndogo zilizojitokeza ikizingatiwa kuwa hiyo ndiyo
safari ya kwanza yatreni hiyo huku akiahidi kuzitafutia ufumbuzi wa
haraka na kuweka hali sawa.
|