Monday, October 22, 2012

WAKRISTO GEITA WACHARUKA WADAI HAWATAVUMILIA KUCHOMEWA MAKANISA

         Habari imeandikwa na MAGRETH CHABA

UMOJA wa Makanisa ya Kikristo ya Katoro wilayani Geita na Buseresere wilayani Chato, mkoani Geita umecharuka na kulaani kitendo cha hivi karibuni kilichofanywa na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislam cha kuchoma moto Makanisa na kuharibu mali za Wakristo.

Kitendo hicho kilisababisha vurugu zilizotokea  Oktoba 12 mwaka huu, huko Mbagala Kizuiani jijini Dar es Salaam ambapo Makanisa saba yalichomwa moto kutokana na kitendo kinachodaiwa na mtoto mwenye umri wa miaka 14 kukojolea Qu’ran.

Umoja huo umetoa tamko kuhusiana na kitendo hicho katika mkutano wa uliofanyika juzi mjini Katoro na kuwakutanisha waumini wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo pamoja na viongozi wao.

Akitoa tamko hilo, mwenyekiti wa umoja huo, Mchungaji Joseph Mwanzalima Hewa, alisema serikali ikishindwa kudhibiti matukio ya vurugu za baadhi ya Waislam kujichukulia sheria mkononi kutokana na udini, Taifa halitakuwa na amani.

Alisema kuna hatari ya Taifa, likaingia katika umwagaji wa damu kwani kwa Wakristo kuzidi kupumbazika kwa kuharibiwa mali zao ni jambo lisilovumilika.

Hewa alisema zaidi ya Biblia 50 ziliwahi kuchomwa moto lakini Wakristo hawakuchukua hatua zozote dhidi ya wahusika wala hakuna Msikiti uliochomwa moto na hakuna vurugu zilizotokea na hivyo kuhoji uhalali wa baadhi ya Waislam kuiweka nchi kwenye rehani ya vita ya kidini.
Alisema Serikali inapaswa kuingilia kati kukomesha matukio hayo yanayofanywa na baadhi ya makundi ya waumini wa dini ya Kiislam ili nchi iendelee kuwa kisiwa cha amani.

Aidha, alisema kama Serikali itashindwa kudhibiti matukio hayo, hawatavumilia kuendelea kuharibiwa Makanisa yao na kudai kuwa wako tayari kufa wakitetea haki zao.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa waliohusika katika matukio hayo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria akiwemo kinara wa kikundi cha Uamsho Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed.

“Serikali imekuwa ikiwakumbatia Waislam, sasa tunasema yatosha. Hatuwezi kuona mali zetu zinaharibiwa. Kama itakuwa kimya katika hili nchi itaingia katika vurugu kubwa na vita kutokana na udini ulioanza kujipenyeza,” alisema Hewa.

Naye aliyewahi kuwa mwenyekiti wa umoja huo, Isaya Ikili alisema anasikitishwa na watendaji wa Kata pamoja na viongozi wa Serikali kushindwa kuhudhuria katika mkutano huo licha kupewa mwaliko ili kujua matamko yao.

Alisema wako tayari kupambana na maadui wao wanaoharibu Makanisa yao na kwamba polisi wasiingilie vurugu hizo kama serikali itashindwa kuyadhibiti