WAKAZI wa Kijiji cha Naisinyai Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara ambao baadhi ya watoto wao waliathirika kwa kupata
ulemavu kutokana na kutumia maji yenye florine,wamezinduliwa mradi mkubwa wa
maji na Mkuu wa mkoa huo.
Mradi huo wa maji ya kisima kirefu ambao
umefadhiliwa na Kampuni ya TanzaniteOne umezinduliwa juzi na mkuu wa mkoa huo
Elaston Mbwilo alipofanya ziara ya kuzindua miradi ya maendeleo kwenye kata ya
Naisinyai.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa
maji,Mbwilo aliwataka wakazi wa eneo hilo kuulinda mradi huo ambao utakuwa na
manufaa makubwa kwa jamii na mifugo iliyopo kwenye eneo hilo.
“Mradi huo unatakiwa kutunzwa kwani kupata
mradi ni jambo linguine lakini kuutumia na kuutunza ni jambo lingine hivyo
utunzeni na pia wapande miti na maua kwa ajili ya kutunza mazingira,” alisema
Mbwilo.
Kwa upande wake,Ofisa Uhusiano msaidizi wa
kampuni ya TanzaniteOne Halfan Hayeshi alisema mradi huo umedhamini na kampuni
yao kwa gharama ya sh milioni 45 na una uwezo wa kutoa lita 30,000 kwa kila
siku.
Hayeshi alisema wameweka mtambo kwenye mradi
huo ambao hutengeneza maji safi na salama yafaayo kwa matumizi ya binadamu na
watauhudumia kwa muda wa mwaka mmoja kisha wataukabishi uongozi wa kijiji uendeleze.
Naye,Mwenyekiti wa Kijiji cha Naisinyai Taiko
Kurian alisema watautunza mradi huo wa maji ambao una manufaa makubwa kwa jamii
tofauti na awali ambapo maji yaliyokuwa yanatumiwa eneo hilo yaliwapa ulemavu baadhi
ya watoto.
Kurian alisema kuwa kupitia mradi huo jamii itanufaika
kwani baadhi ya watoto kabla ya kuanzishwa kwa mradi huo waliathirika kwa miguu
yao kupinda,vichwa kuwa vikubwa na meno kuwa na rangi.