Kipimo cha ‘CT-Scan’ katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
kimeharibika na kusababisha usumbufu mkubwa kwa baadhi ya wagonjwa
wanaoandikiwa kwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kufanyika kipimo
hicho.
Kutokana na hali hiyo, NIPASHE ilishuhudia jana wagonjwa mbalimbali wa
MNH pamoja na wale wanaotoka nje ya hospitali hiyo walioandikiwa kupimwa
kwa kutumia kipimo hicho, wakishauriwa kwenda katika hospitali
nyingine.
Pia NIPASHE ilifika kwenye jengo linalotumiwa kwa ajili ya kipimo hicho
na kumkuta mfanyakazi mmoja aliyekuwa mapokezi, ambaye licha ya kukataa
kutaja jina lake, alijibu kwa kifupi kuwa kipimo hicho kimeharibika kwa
muda mrefu sasa.
Afisa Habari wa MNH, Aminieli Algaesha, hakupatikana ofisini kwake na
hata alipopigiwa simu yake ya mkononi, iliita bila ya kupokelewa.
Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Dk. Merina Njelekela, alipotafutwa kwa njia ya
simu, na kuulizwa kuhusu kuharibika kwa kipimo hicho, hakukiri wala
kukataa, badala yake, aliomba apigiwe baada ya muda mfupi. Hata hivyo,
alipopigiwa simu yake haikuwa na majibu.
CT-Scan iliharibika mwishoni mwa mwaka jana na kutengenezwa katikati ya
mwaka huu, ambapo katika mgomo wa madaktari, wa Februari na Juni mwaka
huu, moja kati ya madai yao, ilikuwa ni kutengenezwa kwa kipimo hicho.
Madaktari hao pia waliitaka serikali kukifanyia kipimo hicho
matengenezo ya haraka na kudai gharama yake ni sawa na gari moja la
kifahari linalotumiwa na mbunge.
source mtandao