Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Bw. Hiiti Sillo akionesha waandishi fomu ya kukusanyia madhara ya dawa (picha: Jiachie blog)
1.0 UTANGULIZI
a). Mamlaka
ya Chakula na Dawa (TFDA) ni Wakala wa Serikali chini ya Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii yenye jukumu la kudhibiti usalama, ubora na ufanisi
wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya ya jamii. TFDA
imeweka mifumo mbalimbali ya udhibiti chini ya sheria ya Chakula, Dawa
na Vipodozi, Sura 219. Mifumo hiyo ni pamoja na usajili wa bidhaa,
usajili wa majengo/maeneo ya kuzalisha na kuuza bidhaa, uchunguzi wa
kimaabara wa sampuli za bidhaa pamoja na ukaguzi na ufuatiliaji wake
kwenye soko.
b). Kupitia
mifumo iliyowekwa, TFDA imekuwa ikihakikisha usalama, ubora na ufanisi
wa dawa katika soko. Aidha, mifumo hiyo pia huwezesha kubaini uwepo wa
bidhaa bandia na duni kwenye soko na kuchukua hatua mbalimbali kwa
mujibu wa Sheria. Hatua hizo ni pamoja na kusitisha matumizi ya bidhaa
husika na kuziondoa kwenye soko, kuziteketeza na kuwafikisha watuhumiwa
kwenye vyombo vya dola na sheria.
c). Itakumbukwa
kwamba, mnamo tarehe 21 Septemba 2012, tarehe 4 Oktoba, 2012 na tarehe
10 Oktoba 2012, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitoa taarifa kwa
umma juu ya uwepo wa dawa bandia ya kupunguza makali ya UKIMWI yenye
jina la kibiashara ‘TT-VIR 30’ toleo Na. 0C.01.85 ikiwa ni pamoja na
hatua zilizochukuliwa. Baada ya taarifa hizi za Wizara kutolewa,
kumekuwa na taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari zinazoleta
mkanganyiko kwa wananchi kuhusu suala hili.
d). Baadhi
ya mikanganyiko hiyo ni pamoja na jinsi dawa hiyo bandia ilivyobainika,
kama barua za TFDA ziliwafikia Tanzania Pharmaceuticals Industries
(TPI) Ltd na kama uzalishaji wa dawa bado unaendelea au la.
e). Ili
kuondoa mkanganyiko ambao umeanza kujitokeza, Mamlaka inapenda kutoa
ufafanuzi zaidi kuhusu dawa hizo bandia ambazo matumizi yake
yamesitishwa. Vilevile, TFDA inapenda kutumia fursa hii kutoa ufafanuzi
kuhusu mfumo wa udhibiti wa dawa nchini.
2.0 UFAFANUZI KUHUSU DAWA BANDIA YA TT-VIR 30
- TFDA
ndiyo iliyobaini uwepo wa dawa bandia aina ya TT-VIR 30 toleo Na.
0C.01.85 kwenye soko mnamo tarehe 28 Julai, 2012 kupitia mfumo wake wa
ukaguzi na ufuatiliaji wa bidhaa katika soko.
- Kama
ilivyoelezwa katika taarifa zilizotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, TFDA inasisitiza kwamba kampuni ya TPI Ltd iliiuzia MSD dawa
bandia aina ya TT-VIR 30 toleo Na. 0C.01.85, kwa mujibu wa nyaraka
zilizopo.
- Nyaraka hizo pamoja na vielelezo mbalimbali zimewasilishwa kwenye vyombo vya usalama kwa hatua zaidi za kisheria.
- TFDA
imesitisha uzalishaji wa dawa za ARVs za kiwanda cha TPI Ltd kupitia
barua Kumb. Na. CA/C.80/222/01A/47 ya tarehe 4 Oktoba, 2012 na vile vile
uzalishaji na usambazaji wa dawa zote kupitia barua Kumb. Na.
CA/C.80/222/01A/55 ya tarehe 10 Oktoba, 2012.
- Barua hizo
zilipelekwa kwa ‘dispatch’ katika ofisi za Makao Makuu ya Kampuni ya TPI
Ltd iliyoko eneo la Mikocheni, Dar es Salaam na kupokelewa tarehe 04 na
10 Oktoba, 2012.
- Taarifa zilizotolewa na Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii zilionesha wazi kwamba TFDA ndiyo iliyositisha
uzalishaji wa dawa katika kiwanda cha TPI Ltd.
- Ukaguzi
uliofanywa na TFDA kwenye kiwanda cha TPI Ltd, Arusha tarehe 12 na 23
Oktoba 2012, umethibitisha kwamba hakuna uzalishaji wa dawa unaoendelea
kwenye kiwanda husika kama ilivyoelekezwa na TFDA.
3.0 MFUMO WA UDHIBITI WA DAWA NCHINI
Aidha, Mamlaka inapenda kutumia fursa hii kufafanua zaidi kuhusu mfumo wa udhibiti wa dawa nchini kama ifuatavyo;
a). Udhibiti
wa dawa unazingatia Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219,
kanuni zilizowekwa, miongozo, misingi ya kisayansi (science based)
pamoja na miundombinu kama vile maabara na mtandao wa ukaguzi. Mifumo ya
udhibiti hujumuisha yafuatayo;-
i. Kufanya tathmini ya taarifa za kisayansi kuhusu ubora, usalama
na ufanisi wa dawa, kufanya ukaguzi wa viwanda na hatimaye kusajili
dawa husika. ii. Kusajili maeneo
yanayojishughulisha na uzalishaji na biashara ya dawa ikiwepo masharti
ya kuwa na wataalam wa kusimamia uzalishaji.
iii. Kufanya ukaguzi wa maeneo yanayotengeneza dawa, vituo vya
forodha pamona na maeneo ya kusambaza na kuuza dawa.
iv. Kufanya ufuatiliaji wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa
zilizosajiliwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba zinakidhi vigezo na
matakwa ya usajili. v. Kufanya
uchunguzi wa kimaabara ili kuhakiki usalama na ubora wa dawa
zinazoombewa usajili na zile zilizoruhusiwa kutumika nchini.
b). Katika
kutekeleza mifumo ya udhibiti na kwa kuzingatia misingi ya udhibiti wa
bidhaa duniani, mwenye jukumu la kwanza la kuhakikisha usalama, ubora na
ufanisi wa bidhaa ni la aliyeisajili bidhaa (marketing authorization
holder) ili kuhakikisha kuwa mtumiaji hapati madhara.
c). Mifumo
hii ndiyo inayoiwezesha TFDA kuhakikisha usalama, ubora na ufanisi wa
dawa na pia kubaini dawa bandia na duni katika soko na kuchukua hatua
kwa mujibu wa sheria.
4.0 HITIMISHO
a). Uchunguzi
zaidi wa dawa bandia aina ya TT-VIR 30 toleo Na. 0C.01.85 unaendelea
kupitia vyombo vya usalama kwa hatua zaidi za kisheria.
b). TFDA
itaendelea kufuatilia usalama, ubora na ufanisi wa dawa kwenye soko
kupitia mifumo iliyowekwa ili kulinda na kudumisha afya ya jamii;
c). Tunapenda
kuwakumbusha wote wanaojihusisha na biashara ya dawa, chakula, vipodozi
na vifaa tiba kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyowekwa na
kwamba yeyote atakayekiuka taratibu hizo atachukuliwa hatua kali za
kisheria.
d). Tunawahakikishia
wananchi kwamba dawa za ARVs zilizoko katika vituo vya kutolea huduma
za afya ni salama na hivyo waendelee kuzitumia bila wasiwasi wowote.
e). Tunatoa
rai kwa vyombo vya habari, watoa huduma za afya na wananchi kuendelea
kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pale wanapobaini au kuhisi kuwepo
kwa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba vyenye mashaka au uvunjifu wa
Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219.
Hiiti B. Sillo MKURUGENZI MKUU MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA 30 OKTOBA, 2012
|