Vipeperushi
vinavyotishia uhai wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar
vimepeperushwa mjini hapa kufuatia ghasia zinazoendelea kwa siku ya tatu
mfululizo.
Kipeperushi kimojawapo kinasema: “CCM kosa letu
kuwatia mbwa msikitini. Sasa tunasema kuwa basi tena litakalokuwa na
liwe kwa sisi CCM basi tena umoja na CUF. Nyie CUF/Muamsho Abubakari
Khamis Bakar (Waziri wa Katiba), Mussa (Kamishna wa Polisi) na Azizi
(Kamanda wa Polisi Mkoa) mmeshazoea fujo na sisi sera yetu CCM sera yetu
amani sasa mujiuzulu mumpishe Rais afanye kazi zake, Tumechoka na
nyinyi juu ya mauaji ya askari wetu. Ondokeni murudi kwenu. Wewe
Abubakar hukuanza leo na jana ufisadi kazi ya ufisadi umeizoweya hadi
ulifungwa jela na mafisadi wenzako, mwishowe huku SMZ kumekuokoa.”
Wakati
huo huo kuna waraka umesambazwa ambao umewatisha hofu waumini wa dini
ya Kikristo nchini ukisema wote watakatwa vichwa. Waraka huo ambao
unasemekana umetolewa na watu wenye kujiita jumuiya ya Uamsho umeandikwa
na kusambazwa katika maeneo mbalimbali huku wenyewe wakristo
wakipelekewa maofisini kwao.
Akizungumza na masikitiko, Askofu
wa Kanisa la Anglikan Mkunazini, Emmanuel Masoud amesema ni wakala ambao
umewastusha Wakristo kutokana na maneno mazito yalioandikwa humo ambapo
ndani ya wakala huo, “Maneno yaliandikwa humu yametushitua sana sisi
waumini wa dini ya Kikristo hapa Zanzibar. Kwa kwa kweli sio jambo la
kupuuzia ikiwa wanasema watatukata vichwa ni jambo la hatari kabisa”
alisema Masoud.
Wakizungumzia ukweli juu ya suala hilo, Sheikh
Azzan amesema Jumuiya yake haihusiki na waraka wa aina hiyo na wao
kama waislamu hawana sababu ya kuwatisha watu kwa kuwa wanaamini Uislamu
sio dini ya kuwabagua watu wala kuwatisha watu.
Azzan alisema
wapo baadhi ya watu ambao wanatumia propaganda mbaya za kutaka kuwagawa
Wazanzibari katika kipindi hiki na ndiyo wanatumia kila sababu za
kuwagawanya. Aliwatahadharisha wananchi kuepukana na propaganda kama
hizo kwani zinaweza kuitia nchi katika pahala pabaya na kutoweka kwa
amani.
“Sisi hatuhusiki na waraka huo aliyetoa waraka huo ni
watu ambao wanapingana na amani iliyopo lakini pia ni watu wenye kueneza
propaganda mbaya za kutaka kuwagawa Wazanzibari, jambo ambalo sisi
tunaamini hatuna ugomvi, na Wazanzibari wote sisi ni ndugu, hatubagui
awe ni Mkristo au Muislam, awe mweupe au mweusi, hatuwezi kubaguana kwa
kuwa misingi ya dini yetu imekataza kubaguana” alisema Azzan.