Wednesday, October 10, 2012

UNAMKUMBUKA YULE DC ALIYESEMA DIGRII YA MWANASHERIA NI YA CHUPI? HAYA NDO YAMEMKUTA JANA

Habari kwa mujibu wa blogu ya Lukwangule -- M AHAKAMA ya Hakimu Mkazi wilaya ya Korogwe jana ilimkataa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kumwakilisha Mkuu wa wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo katika kesi ya madai ya Shilingi Milioni 96 dhidi yake.

Katika kesi hiyo Na. 7/ 2012 mlalamikaji ni Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Najum Tekka anayedai kukashifiwa na Gambo wakati wa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya kwamba stashahada ya Sheria aliyopata mtumishi huyo ni ya chupi.

Awali ilidaiwa kwamba mkuu huyo alimwalika mlalamikaji kutoa ushauri wa kisheria kuhusu namna ya kumaliza mgogoro baina ya halmashauri ya mji na wafanyabiashara na kwamba baada ya kufanya hivyo mlalamikiwa alipinga ushauri uliotolewa na kisha kutoa kauli hiyo kwamba shahada yake ni ya chupi.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Hamis Salum, mlalamikaji huyo aliiomba mahakama imwondoe Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye aliwakilishwa Mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Rebecca Msalangi kwa kuwa hana mamlaka katika madai hayo na kamwe Ofisi yake haikuwahi kupeleka ombi maalum la kutaka kumwakilisha Gambo kwenye shauri hilo.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi akisoma uamuzi mdogo wa Mahakama kuhusiana na mabishano hayo alikiri kwamba utaratibu haukufuatwa na kamwe hapakuwa na ombi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutaka kumwakilisha Gambo kwenye madai hayo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 14 mwaka huu.