|  | 
| Kamishina Wa polisi Musa Ali Mussa akiongea na waandishi wa Habari leo kuhusiana na Vurugu zilizopelekea kifo cha Askari. | 
Na Ramadhan Ali na Mwanaisha Mohammed -Maelezo Zanzibar. 
Askari mmoja
 wa Jeshi la Polisi F.2105 Coplo Said Abdulrahaman wa Kikosi cha FFU 
Mkoa Mjini Magharibi ameuliwa kinyama kwa kupigwa mapanga kichwani na 
mikononi wakati akirudi kazini majira ya saa 6.30 usiku wa kuamkia leo 
katika eneo la Bububu.
Akizungumza 
na waandishi wa habari ofisini kwake Ziwani leo, Kamishna wa Polisi 
Zanzibar, Mussa Ali Mussa amesema mauaji hayo  yamesababishwa na fujo za
 wafuasi wa Jumuiya ya UAMSHO baada ya kuenea uvumi wa kutekwa Msemaji 
Mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Hadi usiku wa kuamkia jana. 
Kamishna 
Mussa amesema Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kuwatafuta watu 
waliofanya mauaji ya Coplo Saidi Abdulrahaman ili kuwakamata na 
kuwafikisha Mahakamani kama  sheria za nchi zinavyowaelekeza.
Amesema 
mpaka hivi sasa watu 10 wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbali mbali 
yaliyotokana na vurugu za jana na upelelezi wa kujua ukweli juu ya uvumi
 wa kutekwa Sheikh Farid unaendelea. 
Ameongeza 
kuwa  kutekwa kwa Sheikh Farid kunatia mashaka kutokana na mazingira ya 
kutoweka kwake kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mdogo wake Said Omar
 Said ambae alikuwa dereva wake katika hatua za mwisho  maeneo ya 
Mazizini walipokwenda kununua umeme.
“Sheikh 
Farid alimuamuru Said amuache katika eneo hilo aende nyumbani kupeleka 
umeme na wakati huo akaendelea na mazungumzo na watu wengine  walikuwemo
 ndani ya gari nyengine ndogo ya NOAH  ambayo nambari zake 
hazijajulikana lakini aliporudi kumchukua hakumkuta” alisema Kamishana 
Mussa.     
Amesema fujo
 hizo zilisababisha hasara  kubwa kwa Serikali, Chama tawala 
na  wananchi ikiwemo kuchoma na kuharibumiundo mbinu ya barabara, 
kuharibu maskani za CCM za Kisonge na Muembeladu kwa kuzichoma moto 
baadhi ya magari kuvunjwa vioo na kuvunja duka la pombe na kuiba mali 
iliyokuwemo ndani. 
Hata hivyo 
amedai hali ya Mji wa Zanzibar kwa sasa ni shwari, wananchi wanaendelea 
na shughuli zao kama kawaida na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na 
vikosi vyengine vya ulinzi na usalama vitaendelea kuhakikisha amani 
inadumu muda wote.
Amewataka 
wananchi kuendelea kuwa wavumilivu na kudumisha amani na utulivu katika 
maeneo yao, na kutoa taarifa za watu waliohusika na  vurugu pamoja 
na  mauaji ya Coplo Said Abdulrahaman. 
 
