Awali, blogu na vyombo mbalimbali vilinukuliwa (bofya hapa kurejea: Taarifa za matokeo ya Chaguzi mbalimbali za Udiwani Oktoba 2012)
vikiripoti kuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, alifyatua
risasi wakati wa uchaguzi wa Kata ya Daraja Mbili huko Arusha.
Habari ifuatayo iliyonukuliwa kwenye gazeti la gazeti la Habari Leo inaripoti kuwa Polisi imekanusha taarifa hizo.
--------------
POLISI
mkoani Arusha imesema kwamba aliyefyatua risasi katika vurugu kwenye
Uchaguzi Mdogo wa udiwani Kata ya Daraja Mbili ni Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), God Mwalusamba na si Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA).
Aidha,
watu 10 ambao ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kuleta vurugu katika
uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili.
Akithibitisha
kufikishwa mahakamani kwa wafuasi hao, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas alisema ni baada ya uchunguzi kukamilika.
Sabas
alisema wafuasi hao walileta vurugu kubwa zilizotokea katika kata hiyo
huku wakiwa na silaha za jadi ambazo ziliwajeruhi baadhi ya vijana wa
Chama Cha Mapinduzi.
Alisema
vurugu hizo zilimfanya Mwalusamba kufyatua risasi nne hewani ili
kuwaokoa baadhi ya vijana wa CCM waliozingirwa na wafuasi wa CHADEMA na
kama isingefanyika hivyo, hali ilikuwa mbaya.
“Unajua
bila Mwalusamba kufyatua risasi nne hewani, hali ilikuwa mbaya sana
kwani vijana wengi wangepata madhara na hata vifo vingetokea, lakini
hatuombi hivyo,” alisema Kamanda Sabas.
Kamanda
huyo alisema katika vurugu zote hizo, walikuwapo Mbunge wa zamani wa
Arusha Mjini, Godbless Lema na Nassari, lakini mbunge huyo wa Arumeru
Mashariki hakupiga risasi yoyote.
Alisema
pamoja na kwamba katika vurugu hizo huwezi kujua nani kapiga risasi
hewani na nani hakupiga, lakini taarifa za kipolisi zimegundua kuwa
Mwalusamba ndiye aliyepiga risasi hewani kuwaokoa vijana wa UVCCM na sio
Nassari.
Kwa upande
wake, Nassari alisisitiza jana kwamba licha ya kuwapo kwenye eneo hilo
mapema juzi asubuhi, hakufyatua risasi, na kwamba taarifa zilizoandikwa
na baadhi ya vyombo vya habari ilikuwa na nia ya kumchafua kisiasa,
lakini kwa imani yake anaamini Mungu atampitisha katika majaribu na vita
hiyo.
Nassari
aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba ni kweli alipita eneo la
Daraja Mbili mapema juzi asubuhi kuwashusha mawakala wa uchaguzi kisha
yeye alikwenda Bang’ata wilayani Arumeru kusimamia uchaguzi kama wakala
mkuu kupitia chama chake hadi usiku wa manane.