MONDAY, OCTOBER 15, 2012TAARIFA KWA UMMA: Madini, Mafuta na Gesi
Spika
wa Bunge Anna Makinda ndani ya wiki moja atumie madaraka na mamlaka
yake kutangaza kwa umma kamati nyingine ya kudumu ya Bunge
itayoshughulikia masuala ya gesi asili kabla na wakati wa mkutano wa
tisa wa Bunge uliopangwa kuanza tarehe 30 Oktoba 2012 kufuatia hali tete
na tata kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini na kwa kuzingatia
umuhimu na unyeti wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya
wananchi.
Pamoja na mambo mengine aelekeze kamati hiyo kupokea
na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge ya mwaka 2011
kuhusu Sekta Ndogo ya Gesi Asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika
kushughulikia tuhuma za ufisadi, madai ya mapunjo ya fedha za mauzo ya
Gesi asili na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango
mkakati na sheria ya gesi asili.
Hatua hii ni muhimu kufuatia
ukimya wa Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo kuhusu
kauli yangu ya tarehe 4 Oktoba 2012 ya kutaka Taarifa ya ufafanuzi
kuhusu utafutaji wa mafuta na gesi asili nchini iliyotolewa na Wizara ya
Nishati na Madini tarehe 21 Septemba 2012 ifutwe kwa kuwa italinda
ufisadi na kukwaza utetezi wa rasilimali za taifa.
Taarifa hiyo
ya Wizara ya Nishati na Madini ilieleza kuwa maandalizi ya sera ya gesi
asili yapo katika hatua za mwisho wakati ambapo kamati mbalimbali za
kudumu za Bunge hazijahusishwa katika mchakato huo muhimu pamoja na kuwa
mamlaka ya kutunga sera kwa mfumo wetu wa sasa ni ya Baraza la Mawaziri
hata hivyo kwa unyeti na upekee wake sera ya gesi Spika wa Bunge
anapaswa kuwezesha Kamati za Kudumu za Bunge zihusishwe ili pawepo
mashauriano na maridhiano kwa mapana na marefu.
Taarifa hiyo ya
Wizara ya Nishati na Madini ilieleza kuwa mikataba 26 ya TPDC ni sehemu
ya nyaraka muhimu za kuboresha utayarishaji wa sera ya gesi asili, hata
hivyo mikataba hiyo imeendelea kuwa siri hivyo Spika aingilie kati
kuziwezesha Kamati za Kudumu za Bunge kuisimamia serikali kurekebisha
mikataba ya sasa na kuboresha mikataba ijayo kwa Serikali kutekeleza
mwito wangu wa toka mwaka 2011 wa kutaka mikataba hiyo iwasilishwe
bungeni na iwekwe wazi kwa umma.
Izingatiwe kwamba katika
Mkutano wa Nane wa Bunge Spika alitangaza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Nishati na Madini imevunjwa na kwamba majukumu yaliyokuwa
yakishughulikiwa na kamati hiyo yatashughulikiwa na kamati nyingine kwa
mujibu wa madaraka na mamlaka ya Spika.
Irejewe kwamba kwa mujibu
wa Kanuni ya 116 na Kanuni ya 114 fasili ya 14 Spika ana mamlaka na
madaraka ya kukabidhi mambo mengine yashughulikiwe na Kamati ya Kudumu
ya Bunge nyingine kama atakayoelekeza.
Ikumbukwe kuwa Julai 2011
na Julai 2012 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na
kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani nilieleza namna nchi yetu
ilivyojaliwa utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi la umasikini wa
wananchi na kwamba taifa letu lina fursa ya kuwa nchi kiongozi katika
gesi Afrika na kushindana kimataifa ikiwa tutaweka mstari wa mbele upeo,
umakini na uadilifu katika sekta ya nishati kuepusha laana ya
rasilimali.
Hata hivyo, mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha
2011/2012 yanaonyesha bado serikali haichukui hatua thabiti
kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi katika sekta ndogo ya gesi
asili hivyo hatua za haraka zisipochukuliwa katika mwaka wa fedha
2012/2013 na kuendelea rasilimali inaweza kuwa chanzo cha migogoro na
kuhatarisha pia usalama wa nchi.
Kwa niaba ya Kambi Rasmi ya
Upinzani nilieleza bungeni tarehe 15 Julai 2011 kuhusu tuhuma za ufisadi
na ukiukwaji wa mikataba katika sekta ndogo ya gesi inaoihusu pia
Kampuni ya Pan African Energy Tanzania (PAT) na kutaka kuundwa kwa
kamati teule ya bunge kuchunguza suala hilo.
Badala yake Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini uliunda kamati ndogo ya
iliyofanya uchunguzi uchunguzi wa masuala husika na taarifa kuwasilishwa
bungeni mwaka 2011 ; hata hivyo mpaka sasa maamizio ya bunge kufuatia
taarifa hiyo hayajatekelezwa kwa ukamilifu.
Tarehe 27 Julai 2012
kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Serikali kueleza ni
kwanini mpaka sasa kiasi cha dola milioni 20.1 zilizopunjwa kifisadi
hazijareshwa na kuitaka serikali iache kutumia kisingizio cha kuundwa
kwa Timu ya Majadiliano (GNT) kuchelewesha utekelezaji wa maazimio,
suala ambalo Wizara ya Nishati na Madini itapaswa kueleza hatua
iliyofikiwa iwapo Spika atazingatia mwito huu na kuchukua hatua za
haraka.
Ifahamike pia kwamba mwaka 2011 kwa nafasi yangu ya
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini niliitaka serikali ambazo kuweka
wazi bungeni na kwa umma mikataba ya madini, mafuta na gesi asili katika
nchini ili kuongeza tija na uwajibikaji.
Aidha nilitoa mwito
mwito kwa wananchi na wabunge kuongoza marekebisho ya kikatiba na
kisheria ili kuweka vifungu vya kulazimisha uwazi katika mikataba katika
hizo muhimu kwa uchumi na usalama wa nchi.
Uwazi katika mikataba
utadhibiti pia mianya ya ufisadi miongoni mwa baadhi ya watendaji wa
serikali kwa kuwa mikataba hiyo itajadiliwa na umma na hivyo kupunguza
uwezekano wa viongozi kutanguliza maslahi binafsi na kuwa na mikataba
bora ya baadaye yenye kuzingatia maslahi ya umma.
Usiri katika
mikataba ni tatizo kwa sababu masharti kama ya kushughulikia madhara ya
kimazingira na kuchangia katika huduma za jamii pamoja na kulipa kodi
zinazokusudiwa yanaweza yasitekelezwe kwa ukamilifu kama hayatafahamika
kwa wabunge na umma. Aidha, ipo mikataba yenye vifungu ambavyo
vinakinzana na sheria nyingine ama vinalinda kupindukia makampuni dhidi
ya sheria nyingine za nchi zinazotungwa masuala ambayo yanaingilia
mamlaka ya bunge ya kutunga sheria na kuisimamia serikali.
Sheria
mpya ya madini Tanzania ya mwaka 2010 ina kifungu kinachotaka uwazi
hata hivyo kimejikita katika uwazi wa rekodi na ripoti hakijaweka bayana
mfumo wa uwazi katika mikataba ya madini, sheria ya mafuta nayo haina
kifungu cha uwazi katika mikataba na sheria ya gesi haipo kabisa; hali
ambayo inahitaji kurekebishwa.
Pamoja na mapato uwazi katika
mikataba utachangia katika kupata tija ya ziada katika uchimbaji kwa
kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuweka mfumo mzuri zaidi wa makampuni
kununua bidhaa za ndani kwa majibu wa vifungu vya mikataba hali ambacho
itawezesha rasilimali kunufaisha wananchi wengi zaidi.
Uwazi
katika mikataba utawezesha wabunge na wadau wengine kusimamia ipasavyo
taasisi za kiserikali kuhusu mifumo ya kifedha na kibenki ambayo
itaongeza mchango wa sekta za nishati na madini katika kuimarisha
uchumi kwa kudhibiti mfumuko wa bei na kuporomoka kwa sarafu wakati huu
ambapo thamani ya mauzo imeongezeka duniani lakini mzunguko umejitika
katika masoko na mabenki ya nje. Kwa ujumla, uwazi katika mikataba
utapanua pia uwajibikaji wa kuongeza umiliki wa nchi na wananchi wa
michakato ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili.
Pamoja
na kuwa ibara ya nne ya katiba inasema kwamba rasilimali na mali asili
zote ziko chini ya usimamizi wa serikali; na ibara ya 63 inaeleza kwamba
bunge ndicho chombo kikuu cha kuisimamia serikali kwa kutunga sheria na
kupitisha mipango, katiba haijalazimisha mikataba ya madini, mafuta na
gesi kuridhiwa na bunge hivyo katika kipindi cha sasa mikataba hiyo
iwasilishwe kwa rejea na mapitio.
Katika muktadha huo, tarehe 4
Oktoba 2012 nilimtaka Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo
afute taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwa lengo la
agizo lake la kupitiwa kwa mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta na gesi
asili ni “kuhakikisha kwamba endapo kuna mapungufu katika mikataba hiyo,
mapungufu hayo yasijirudie tena katika mikataba mipya ya baadaye” kwa
kuwa ikiachwa ilivyo italinda ufisadi na kukwaza utetezi wa rasilimali
za taifa.
Nilieleza kwamba ufafanuzi uliotolewa na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini unatoa mwanya kwa mikataba mibovu kulindwa
wakati ambapo kuna madai tuliyotoa toka mwaka 2011 kwamba baadhi ya
mikataba hiyo imeingiwa kifisadi na mwaka huu wa 2012 zimeibuka tuhuma
za vigogo wa serikali kuingiziwa fedha kifisadi katika akaunti zao za
nchini Uswisi na makampuni ya nje ya utafutaji mafuta na gesi asili.
Aidha,
pamoja Serikali kuwasilisha bungeni mikataba inapaswa pia kuwasilisha
mipango kabambe (master plan) ya mafuta na gesi asili yenye kuzingatia
mabadiliko ya kisera na kimfumo yenye kuwezesha nchi na wananchi
kunufaika na rasilimali husika.
Kauli hii nimeitoa leo tarehe 14
Oktoba 2012 ikiwa ni Siku ya Kumbukumbu ya Hayati Julius Nyerere ambaye
alipinga ufisadi na kutaka rasilimali za nchi zitumike kwa manufaa ya
maisha ya wananchi:
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini