Kamati ya Bunge inayoshughulikia masuala ya Ukimwi imeishauri serikali
kutoa tamko la kuelezea ni hatua gani inaendelea kuchukua baada ya
kusimamisha kazi baadhi ya viongozi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kufuatia
kuwepo kwa dawa bandia za kupunguza makali ya UKIMWI ( ARV) katika
kikao cha Bunge kitakachoanza mwishoni mwezi huu.
Kauli hiyo
imetolewa leo na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Lediana Mng’ong’o wakati
akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini
Dares Salaam kuhusu kuwepo kwa dawa hizo.
“Sisi tungependa
kuishauri serikali kuendelea kufuatilia na hatua za kisheria pale
itakapobaini katika uchunguzi huo ili tatizo hili lisiendelee kutokea,”
alisema Lediana ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Iringa.
Aliongeza
kuwa wanaishauri Mamlaka cha Chakula na Dawa (TFDA) kuwa na wawakilishi
katika kanda mbalimbali ili kuweza kudhibiti tatizo la kuwepo kwa dawa
bandia.
Aidha kamati hiyo imelaani kampuni ambayo imeingiza dawa feki na imetaka hatua za kisheria zichukuliwe.
Kamati
hiyo imewataka watu wanaotumia dawa hizo kutoziacha , bali waendelee
kuzitumia kwa kuwa dawa zote si feki na pia zipo za kutosha.