Hospitali ya Taifa Muhimbili imeandaa mkutano na wadau utakaofanyika Oktoba 9, 2012 saa 04:00 asubuhi katika ukumbi wa Karimjee.
Lengo
la mkutano huu ni kutaka kupata maoni ya moja kwa moja kutoka kwa
wananchi tunaowahudumia kuhusu kuridhika au kutoridhika kwao na huduma
tunayotoa. Wananchi wataeleza ni maeneo gani hawaridhiki nayo na pia
watapata fursa ya kushauri nini kifanyike ili kuboresha huduma za tiba,
uchunguzi, upasuaji n.k
Hospitali inatoa huduma kwa wagonjwa wa
nje wasiopungua 1,000 hadi 1,200 kwa siku na wagonjwa waliolazwa kwa
wakati wote wodini ni kati ya 1,000 hadi 1,200 kwa siku.
Hospitali imeonelea ni wakati muafaka wananchi kutumia fursa hii kushiriki katika mkutano huu kutoa maoni yao moja kwa moja.
Mkutano
huu utahudhuriwa na Menejimenti ya Hospitali ikiongozwa na Mkurugenzi
Mtendaji ambayo ndiyo yenye dhamana na kusimamia utendaji wa kila siku
wa Hospitali.
Wakuu wa Idara zote ambazo huduma zinatolewa katika
maeneo yao watakuwepo katika Mkutano huo ili kusikia moja kwa moja
kutoka kwa wananchi juu ya utendaji wa idara zao kwa wananchi
wanaowahudumia.
Tunaomba kuchukua fursa hii, kwa dhati kabisa
kuwaalika wananchi kufika na kushiriki kikamilifu katika mkutano huu ili
kutoa maoni yao. Tunaamini kuwa maoni yao ni ya muhimu sana na ndiyo
maana tumetoa fursa hii ili tupate mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa
wadau tunaowahudumia.
Kama kuna swali lolote ambalo mwananchi angependa kuuliza kabla ya mkutano huo anaweza kutuma kupitia barua pepe info@mnh.or.tz nasi
tutalifanyia kazi na kutoa majibu siku hiyo hiyo ya mkutano. Aidha
unaweza kutuma maoni yako kwa njia ya posta kwa Mkurugenzi Mtendaji,
Hospitali ya Taifa Muhimbil, S. L. P. 65000 Dar Es Salaam. Tutaipokea
barua yako na tutaijibu.
Ndugu wananchi, tunarudia tena kuwaomba
kushiriki kikamilifu katika mkutano huu ili kutoa maoni yenu juu ya
huduma mablimbali zitolewazo na hospitali ya taifa. Karibuni sana..
Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano
Hospitali ya Taifa Muhimbili
Oktoba 4, 2012