Sunday, October 14, 2012

HABARI KUHUSU KIFO CHA KAMANDA BARLOW

Tetesi zinaeleza kwamba, tukio la kuuawa kwa Kamanda huyo huenda limesababishwa na uhasama na watu mbali mbali katika maeneo ya kazi alikowahi kufanyia, na kwamba hilo ni tukio linalotia shaka iwapo kama imetokea kwa bahati mbaya.

Baadhi ya watu wanalihusisha tukio hilo na mahusiano ya kimapenzi, misimamo yake mikali ya kupambana na majambazi, ambapo alikuwa akitoa onyo kwa majambazi kutoingia katika eneo lake la kazi.  

Kwa upande wao, watoto wa Doroth Moses walisema kwamba siku ya tukio mama yao aliwaaga jioni kuwa anakwenda katika kikao cha harusi cha rafiki yake, na wakati anarudi nyumbani  majira ya saa 4 usiku aliwapigia simu ili wamfungulie geti, na kwamba wakati mtoto mmoja Keny Rogers (17), akienda  kumfungulia geti aliona kundi la watu kama watano wakiwa wamezunguka gari.

“Yule mwanaume (RPC), aliyekuwa amemleta mama (Doroth), sisi hapa hatumjui na hata hatujawai kumuoana. 

Lakini mama alitupigia simu akisema tumfungulie geti..

“Wakati mimi nimeenda kufungulia geti, niliona kundi la watu watano lakini mimi hawakunioana. Wakati naendelea kuwacheki (kuwaangalia), kama nawafahamu ama lah, ghafla nikasikia mlio wa bunduki kisha wale watu wakakimbia. Nikaanza kuona damu nyingi zinamwagika chini”, alisema mtoto Keny.

Awali iliripotiwa kwamba Doroth alikua ni dada wa marehemu Barlow.

Hili ni miongoni mwa matukio makubwa  ambayo yameripotiwa kutokea jijini Mwanza, ambapo hivi karibuni iliarifiwa kwamba, Ofisa mmoja wa Uhamiaji Mkoani Mwanza, Albert Buchafwe alinisurika kuuawa kwa risasi na mtu anayedaiwa kuwa ni Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi cha Nyakato Mwatex (OCS), Abubakar Zebo baada ya kushukiwa kuwa ni jambazi.

Ilidaiwa kwamba, Ofisa huyo wa Uhamiaji alifyatuliwa risasi tano wakati akijaribu kukimbia, na kwamba gari lake liliumizwa vibaya na risasi zilizokuwa zikifyatuliwa na OCS Abubakar, na kwamba tukio hilo lilithibitishwa na Ofisa huyo wa Uhamiaji pamoja na marehemu RPC Barlow.

Tukio jingine lilitokea miezi michache iliyopita, ni lile la mwanasiasa maarufu jijini hapa, Seni Manumbu aliyeuawa kwa kupigwa risasi za moto na watu wasiojulikana, wakati alipokuwa akifunguliwa geti ili aingie nyumbani kwake.

---
Sehemu hii ya taarifa imenukuliwa kutoka kwenye habari ilivyoandikwa na Sitta Tumma kwenye FikraPevu – Mwanza.
                                                                                           -------------- xxxxx----------------

Mwandishi alifika eneo la tukio na kuzungumza na mtoto wa kaka wa Mwalimu Moses anayeitwa Kennyrogers Edwin aliyedai kuwa muda mfupi kabla ya tukio, mwalimu huyo aliwapigia simu akiwataka wamfungulie.

Alipofungua lango, aliona gari limepaki na watu wawili wakiwa upande wa abiria na wengine kwa dereva na alisikia mlio wa risasi na kushuhudia watu hao wakikimbia baada ya kuona pikipiki inakuja nyuma yao.

Mmoja wa wakazi wa Kitangiri, Edward Jackson ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu sekondari ya Kitangiri alisema akiwa mezani anajisomea usiku alisikia mlio wa risasi na alipotaka kutoka nje mama yake alimzuia ili asije akadhurika.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, licha ya kushitushwa na kuhuzunishwa na tukio hilo, alitaka wananchi kutoa ushirikiano ili kubaini wahusika. 

Mwili wa Barlow ulifikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kati ya saa 8.30 na tisa alfajiri na kufanyiwa uchunguzi na madaktari na kisha kuhifadhiwa katika mochari ya hospitali hiyo.

Mmoja wa madaktari ambao walimpokea na kumfanyia uchunguzi wa awali walisema jeraha la risasi lililosababisha kifo cha Kamanda huyo liliharibu mfumo wa mawasiliano baada ya kumvunja shingo. 

“Hakika ni moja ya vifo vya kutisha ambavyo nimewahi kuvishuhudia tangu niwe daktari, hata wenzangu tuliokuwa nao tulibaki tunashangaa kuona kiongozi mkubwa anakatishwa maisha kwa risasi,” alisema mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Baadhi ya wananchi waliozungumza kwa nyakati tofauti, walionesha masikitiko yao kutokana na kifo cha Kamanda Barlow.

Walisema katika kipindi alichokaa hapa alifanikiwa kudhibiti ujambazi kutokana na kusimamia doria za mara kwa mara jijini hapa na atakumbukwa kwa jinsi alivyosimamia mauaji ya majambazi watano walivamia duka katikati ya Jiji.

“Tumepoteza jembe halisi na mwana wa Tanzania, Kamanda Barlow alifanikiwa kusimamia haki na kukomesha ujambazi, tunaliomba Jeshi la Polisi mkoani hapa lihakikishe linawatia nguvuni wahusika wote,” alisema Patricia Jumbe mkazi wa hapa.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Lily Matola alisema wanamshikilia mwanamke aliyekuwa na Kamanda huyo kwa mahojiano ili kujua chanzo cha mauaji hao.

“Tunamhoji mwanamke huyo na kufanya uchunguzi wa kina, tutatoa taarifa baada ya kufanya uchunguzi wa awali na suala la mazishi tunasubiri maelekezo ya kaka wa marehemu aliye Dar es Salaam,” alisema.

---
Sehemu hii ya taarifa imenukuliwa kutoka kwenye habari iliyoandikwa kwenye  blogu ya Ziro & Tina