Tunapongeza matamko yaliyotolewa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete na
viongozi wa dini ya Kiislamu nchini Tanzania wakilaani kushambuliwa kwa
wanadiplomasia wa Kimarekani huko Libya na vitendo vingine vilivyo
kinyume na imani za kidini, huku wakihimiza kuwepo kwa utulivu na
majadliano ya amani.
Ikiwa nchi ya watu wa imani zote, wakiwemo
mamilioni ya Waislamu, Marekani inaamini kwa dhati kabisa katika uhuru
wa watu kuabudu na kufuata imani zao za kidini. Kama alivyosema Waziri
wa Mambo ya Nje wa Marekani Bibi. Hillary Rodham Clinton siku ya Ijumaa,
Septemba 14, 2012, Serikali ya Marekani haihusiki kwa vyovyote vile na
filamu ya udhalilishaji inayosambazwa katika mtandao wa internet ambayo
ndiyo imesababisha maandamano katika nchi mbalimbali. Tunapinga na
kulaani maudhui yake yasiyo na chembe ya heshima na ujumbe wake wa
kuudhi na kuleta chuki.
Marekani na Tanzania ni nchi zenye hazina
kubwa ya kuheshimu uhuru wa dini na watu wake wa dini mbalimbali
kuvumiliana. Ubalozi wetu jijini Dar es Salaam una fahari kubwa
kushirikiana na viongozi wa dini zote. Programu za kujenga maelewano, na
mabadilishano ya kitamaduni na kielimu na Watanzania wa imani zote,
ikiwemo Waislamu, ni jambo linalopewa kipaumbele cha juu na Ubalozi wa
Marekani nchini Tanzania.
Programu zetu za kusaidia maendeleo
zinatuwezesha kufanyakazi na viongozi wa kidini, mashirika ya kiraia na
sekta binafsi na kusaidia jitihada zao za kujenga mustakabala Mwema kwa
Watanzania wote.
Kwa mfano, kwa kupitia Millennium Challenge
Corporation (MCC), serikali ya Marekani inafadhili mradi wa kupeleka
Zanzibar umeme wa megawati 100 kupitia nyaya zinazolazwa baharini ili
kuboresha upatikanaji wa umeme visiwani humo. Kwa kupitia Shirika la
Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) mradi wa kutokomeza Malaria
visiwani Zanzibar umepunguza kwa kiwango kikubwa matukio ya ugonjwa huo
Zanzibar.
Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na
UKIMWI (PEPFAR) umekuwa ukiendesha programu mbalimbali za kukabiliana
na VVU/UKIMWI zinazookoa Maisha ya maelfu ya watu nchini Tanzania. Hali
kadhalika, Mpango wa kusaidia kilimo na usalama wa chakula unaoendeshwa
na USAID (Feed the Future) unafadhili shughuli mbalimbali za kilimo na
kiuchumi zinazolenga kuinua ubora wa Maisha wa Watanzania wote - ambao
miongoni mwao Waislamu ni sehemu kubwa.
Katika kujenga na
kuimarisha mahusiano baina ya watu wa nchi hizi mbili, Ubalozi wa
Marekani umekuwa ukiwakaribisha vijana wa Kiislamu katika maktaba yake
kuu na katika maktaba ndogo (American Corners) zilizopo Unguja, Pemba na
Mwanza.
Aidha, Ubalozi umekuwa ukiendesha programu mbalimbali
za kuwafikia Watanzania huko waliko (outreach programs) na kuwa na
majadiliano nao yaliyo wazi. Mfuko wa Balozi wa Marekani wa Kuhifadhi
Amali za Kitamaduni (The Ambassador's Fund for Cultural Preservation)
umekuwa ukitupa fursa ya kuonyesha jinsi Marekani inavyoheshimu na
kuthamini hazina ya kipekee ya kitamaduni na kihistoria ya Tanzania.
Toka
mwaka 2002, Watu wa Marekani wametoa jumla ya Dola za Kimarekani
1,090,000 katika kusaidia hazina za kiutamaduni na kihistoria za
Tanzania, ikiwa ni pamoja na Miskiti ya Kizimkazi na Micheweni huko
Zanzibar na magofu ya Kilwa Kisiwani. Hali kadhalika, Watu wa Marekani
wametoa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 49 kuchangia mradi wa
matumizi ya teknolojia ya kisasa ya habari katika kufundishia mashuleni
(Tanzania 21st Century Education Program -TZ21) unaotekelezwa huko
Zanzibar na Mtwara kupitia USAID.
Kukuza majadiliano ya wazi na
ukweli pamoja na kujenga maelewano ndiyo dhamira yetu kuu. Tumedhamiria
kwa dhati kufanyakazi na Watanzania katika kuendeleza malengo hayo.
----
Tamko limenukuliwa kutoka, SwahiliVilla blog