Saturday, September 29, 2012

MEMBE AIAMBIA UN KUWA TANZANIA HAITAPIGANA NA MALAWI

SERIKALI ya Tanzania imeuambia rasmi Umoja wa Mataifa (UN) kamwe haitaingia vitani na Malawi baada ya kuibuka mgogoro wa mpaka unaohusisha nchi hizo mbili katika Ziwa Nyasa.

Badala yake, itawasilisha madai yake katika Mahakama ya Kimataifa yenye dhamana ya utatuzi wa mgogoro iliyo chini ya Umoja wa Mataifa ambayo itakuwa mwamuzi wa mwisho wa uhalali wa mpaka huo.

Hayo yalisemwa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa 67 wa Umoja wa Mataifa (UN) unaoendelea jijini hapa, akimwakilisha Rais Jakaya Kikwete.

Alisema Tanzania imekuwa mpatanishi mkuu wa migogoro duniani ukiwamo wa Burundi uliokuwa ukisimamiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na kamwe haitakuwa kielelezo kibaya cha kudai inachokiamini kwa kutumia nguvu, “Ushiriki wa marais wetu wastaafu kuanzia Mwalimu Nyerere, Benjamin Mkapa na Rais Kikwete kutatua migogoro mbalimbali, hivi sasa ni sababu tosha ya kuifanya dunia iamini kuwa njia sahihi kwa Tanzania kutatua mgogoro ni diplomasia,” alisisitiza Membe.

Kuhusu migogoro inayoendelea duniani, Membe alisema kushindwa kuvumiliana kwa wanaopingana katika nyanja tofauti kumekuwa sababu kuu ya migogoro hiyo kukithiri na kuhatarisha usalama wa watu na mali sehemu husika.

Katika mkutano huo, Membe aliuomba Umoja wa Mataifa kutafuta njia ya dharura ya kutatua mgogoro unaoendelea Syria kati ya majeshi ya Serikali na yanayompinga Rais Bashir al Asad kutokana na athari kubwa iliyojitokeza katika Taifa hilo hadi sasa, “Mheshimiwa Rais wa Baraza hili, sisi sote tunajua madhara ya migogoro na vita, hasa pale maazimio ya UN yanapokiukwa, hali ya Syria ni moja kati ya mifano hiyo ni vema tukawa makini kufikiria mapema njia za kutatua migogoro kabla ya madhara kama hayo kujitokeza,” alisema Membe.

Katika mkutano huo, Membe alisema Tanzania na nchi nyingine 12 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimekubaliana kuunda Jeshi la pamoja na kukituma kikosi cha askari 4,000 na kulituma Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC) kusaidia upatikanaji wa amani ya kudumu dhidi ya waasi wa M23 wanaoipinga Serikali ya nchi hiyo.

---
Habari via HabariLeo