Thursday, September 27, 2012

KISA CHA MWANAFUNZI FIKIRI

Fikiri ni mwanafunzi katika shule ya sekondari Mabadiliko. Yuko kidato cha pili.

Shule ya sekondari Mabadiliko imekuwa na uhaba wa walimu. Katika masomo tisa anayosoma Fikiri ni masomo matatu tu yenye walimu, ambayo ni hisabati, jiografia na kiswahili. Masomo haya pia yamepatiwa vitabu vya kutosha kwa sababu rasilimali zote za shule hiyo zinaelekzwa kwenye masomo hayo yenye walimu.

Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mabadiliko anategemea mwaka ujao wa fedha walimu watakubali kuja kufundisha shuleni hapo kwa kuwa tarafa yao kwa mara ya kwanza itapata nishati ya umeme. Vilevile tayari kijiji kimeshapatiwa kisima cha maji. Ukosefu wa maji na umeme uliwafanya walimu kukataa kabisa kupangiwa kazi katika shule ya Mabadiliko.

Fikiri amekuwa akirudia kidato cha pili kwa miaka miwili sasa. Ameshindwa kupata alama za wastani wa kumuwezesha kuingia kidato cha tatu. Wanafunzi wengine wamefanikiwa kupata alama hizo na wanaendelea katika vidato vya juu.

Wazee wa kijiji wanafahamu kuwa Fikiri hatilii maanani masomo yake. hivyo waliamua kumuweka chini na kumhoji. Alipoulizwa sababu za kushindw kupata wastani wa kuendelea kidato cha tatu, Fikiri alisema kuwa swali hilo linamtia hasira. Amesema hali ya shule yao kukosa walimu kila mtu anaifahamu na kwanini washangae yeye kukosa wastani wa kufaulu. Katika mitihani yake Fikiri hupata F za masomo nane na D ya somo la Kiingereza.

Tangu kipindi hicho Fikiri amejenga chuki na wazee wa kijiji cha Mabadiliko na amekuwa akilaani kitendo chao cha kumuona yeye mzembe wakati wanajua hali ya uhaba wa walimu ilivyo. Fikiri amejitoa katika kushiriki shughuli za maendeleo kijijini na marafiki zake wengi amegombana nao.

Somo: Pamoja na shule ya mabadiliko kukosa walimu wa masomo mengine, lakini uwepo wa walimu wa Hisabati, jiografia na kiswahili ulipaswa kutumiwa ipasavyo na Fikiri katika kujiendeleza kimasomo na kupata wastani wa kuendelea vidato vya juu.

Fikiri alitoa kipaumbele zaidi kwenye kulalamikia udhaifu uliopo ambao kwa kiasi kikubwa uko nje ya uwezo wake kuutatua badala ya kuzingatia zaidi nafasi yake katika kutekeleza wajibu wake.

Je, walimu wa masomo mengine wakiripoti Fikiri atabadilisha tabia yake na kuanza kufanya bidii? au tabia hiyo itakuwa ndio mfumo wake wa maisha na atakachofanya ni kutafuta sababu nyingine ya kulalamika