SIKU chache baada ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
kufichua ufisadi wa Tsh bilioni 30 kwa mwezi zilizokuwa zikiliwa na
wajanja kupitia Tanesco huku Zitto Kabwe akiwa miongoni mwa
wabunge waliotuhumiwa ufisadi huo Zitto ambaye ni Mwenyekiti
wa kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma amevunja ukimya na kuweka mambo
hadharani.
HAYA NDIYO YALIYOSEMWA NA ZITO KABWE
Nalazimika kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo
la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki katika
vitendo vya rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Mashirika ya Umma. Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote
zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma.
Nafahamu nabeba dhamana kubwa ya uongozi,
taswira yangu ya uongozi daima imeakisi njozi na matumaini ya wananchi wa
Kigoma Kaskazini, wananchi wanyonge na vijana kote nchini bila kujali itikadi
zao za kisiasa, jinsia zao, makabila yao na rika zao. Hivyo, nawajibika kupitia
kwenu kuwatoa hofu juu ya hisia potofu zinazopandikizwa kwao na wale wasiopenda
kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na kuwasemea watanzania wasio na sauti, dhidi
ya vitendo vya hujuma na vyenye dhamira ovu kwa taifa.
Mkakati huo wa kuniunganisha na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge
wanaotuhumiwa kwa kupokea Rushwa unatekelezwa kwa njia zifuatazo:
1. Kumekuwa na kauli za watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza na
hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli zangu zinatokana na ushawishi wa
rushwa.
2. Kuna taarifa ambazo zimeandikwa tena katika kurasa za mbele za baadhi ya
vyombo vya habari zikidai ’’Zitto kitanzini’’ ama ’’Zitto sawa na popo
nundu’’ zikiashiria kwamba na mimi ni mla rushwa; na
3. Waandishi wa habari na jamii kwa ujumla wamefikia kuaminishwa habari hizi
kiasi cha wengine kuuliza kwa nini Mhe. Zitto Kabwe hakutajwa katika orodha
iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani.
Naomba kutoa ufafanuzi wa hicho kinachoelezwa kwamba nina ushiriki katika
masuala ya rushwa hususan kwenye masuala yanayohusu sekta ya Nishati na
Madini:-
1. Mara baada ya bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Usambazaji wa Umeme
Tanzania (TANESCO) chini ya Uenyekiti wake Meja Jenerali Mstaafu Robert Mboma
kutangaza kwamba imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nd.
William Mhando ili kupisha uchunguzi wa baadhi ya vitendo/mwenendo wake, Kamati
ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo mimi ni Mwenyekiti wake
ilimuandikia Mhe. Spika kumuomba aridhie ili Kamati iweze kuwaita Bodi ya
TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) na pia
Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote
zinazotajwa zinafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa;
2. Kamati ya POAC ninayoiongoza ilimuomba Mhe. Spika kuwaita wahusika tajwa kwa
kuwa zilikuwapo tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi huyo siku chache
kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika
’madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao
naona umefanikiwa sana. Isitoshe, Kamati kutaka kujiridhisha na hatua za Bodi
ni sehemu ya msingi ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati yaliyowekwa kwa mujibu
wa Kanuni za Kudumu za Bunge na pia Shirika la TANESCO ni moja kati ya
mashirika ambayo yanawajibika kwetu kwa hesabu zake na pia ufanisi wake kwa
ujumla. Tumefanya hivyo pia katika mashirika mengine, hili la TANESCO sio tukio
la kipekee;
3. Kitendo hiki cha halali na kwa mujibu wa Kanuni kilichofanywa na Kamati yangu
kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa sisi au
zaidi kwamba mimi nina maslahi binafsi na TANESCO na hususan Mkurugenzi wake
Injinia Mhando, ndio maana tumetaka maelezo ya Bodi. Ukweli kwamba Kamati ya
POAC tumewaita pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu (CAG) na Mamlaka ya
Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa jambo hilo hilo umefichwa kwa makusudi!
4. Baada ya tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti
moja alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu
wake, Nd. Eliachim Maswi hapa hapa Bungeni na wamewaambia kuwa mimi nimepewa
rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala kwa lengo gani!
5. Nimejaribu kumtafuta kwa simu Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake ili
wanipe ufafanuzi juu ya mimi na Kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma hizi bila
mafanikio, hali ambayo inaniondolea mashaka juu ya ushiriki wao katika kueneza
au kuthibitisha uvumi huo. Najaribu sana kujizuia kutokuwa na mashaka na
ushiriki wao huo ikizingatiwa uzito na taswira ya nafasi zao katika jamii,
lakini wameshindwa kunidhihirishia tofauti.
Sasa naomba kutoa ufafanuzi rasmi kuhusu mlolongo wa matukio hayo tajwa ambayo
yanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kuonesha kwamba eti nimehusika na vitendo vya
rushwa.
1. Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yeyote na uongozi wa TANESCO
kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka kujiridhisha
juu ya utaratibu uliotumika. Ieleweke wazi kabisa kuwa, hakuna wakati wowote,
popote ambapo mimi binafsi au Kamati yetu imekataa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO
kuchunguzwa kwa tuhuma zozote. Ambacho tumesisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa
taratibu, kanuni na sheria, hili nitalisimamia iwe masika au kiangazi;
2. Ni kwa sababu hiyo, na kwa kujiamini kabisa nimeunga mkono suala la tuhuma
za rushwa zinazotajwa zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge kwa kina;
3. Nimekwenda mbali zaidi kukiomba chama changu CHADEMA kifanye pia uchunguzi
na tathmini yake kwa kina kujiridhisha na tuhuma hizo;
4. Natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya Dola vichunguze tuhuma hizo kwa
nafasi yake ili kuweza kupata ukweli;
5. Ninaahidi kushiriki kikamilifu iwapo nitatakiwa katika uchunguzi wowote
utakaofanywa na niko tayari kuwajibika iwapo nitakutwa na hatia yeyote.
Napenda niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Kigoma Kaskazini walionituma kuja
kuwawakilisha hapa Bungeni na Watanzania wote kwa ujumla kwamba:-
|