Gazeti
la habari leo la tarehe 5 Agosti, 2012 liliripoti kwamba, mkazi mmoja wa kijiji
cha Mubinyage Ngara mkoani Kagera, Adam Balekawe (32) alidaiwa kufanya mauaji
ya kinyama kwa kumchoma sindano ya sumu na kumnywesha sumu mtoto wake mwenye
umri wa miezi tatu, Amani Adam, akihofia kuchekwa na ndugu kwa kuzaa na
Ombeni Paschal (27) mwanamke mwenye ulemavu.
Wizara
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imesikitishwa na taarifa ya mauaji ya
mtoto huyo mdogo asiyekuwa na hatia. Aidha, Wizara imesikitishwa na
sababu za unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu jambo ambalo limepelekea mtoto
huyo kuuawa na baba yake kwa kuwa tu mama wa mtoto ni mlemavu.
Wizara
inakemea na kulaani vikali mauaji ya mtoto huyo na inapenda kusisitiza kwamba
watu wenye ulemavu wanayo haki na nafasi katika jamii sawa na watu wengine.
Vilevile jamii itambue kuwa watu wenye ulemavu wanahaki ya kuthaminiwa utu wao
na kushiriki haki zote za msingi. Aidha, kitendo kilichofanywa na baba wa mtoto
huyo kimechochewa na mazingira na mitizamo finyu katika jamii kuhusu walemamvu
jambo ambalo linachangia unyanyapaa kwa kundi hili ambao unasababisha kutengwa
kwao katika maisha na shughuli za kila siku katika jamii zetu. Wizara inapenda
kueleza kuwa mtizamo huo ni hasi na unakwenda kinyume na haki za binadamu hivyo
ni budi wananchi kuachana na mila na imani zenye ukatili wa kupokonya haki ya
ambayo ndio haki kuu zaidi ya haki zote.
Katika
tukio lingine imeripotiwa kuwa mkazi wa kijiji cha Ndelema Crispin Lwela (26)
anadaiwa kumbaka kisha kufanya mauaji ya kinyama kwa kumchinja na kisu mtoto
wake mwenye umri wa miaka mitatu. Wizara imesikitishwa na tukio hilo na
kwa msingi huu Wizara inapenda kuwakumbusha wananchi kwamba Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inasisitiza kwamba binadamu wote ni sawa na kwamba
wanastahili kupata haki sawa bila kujali rangi, kabila na dini.
Mwisho
Wizara inaendelea kuhimiza jamii kubadilika na kuhakikisha kuwa familia
zinakuwa salama na mahali penye amani miongoni na wanafamilia bila kusahau
kulinda na kuendeleza haki za watoto wote katika jamii. Vilevile Wizara inatoa
pole kwa mama Ombeni Paschal ambaye amefiwa na mtoto wake mwenye umri mdogo
kutokana na kufanyiwa ukatili na baba yake. Aidha Wizara inaomba mama wa mtoto
na wanafamilia wote kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha majonzi.
Erasto T. Ching’oro
MSEMAJI WA WIZARA
08
Agosti, 2012
|