Dodoma -- POLISI wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya umati wa watu uliokataa kuhesabiwa wilayani Kongwa wakishinikiza waganga wa jadi waliokuwa wakishikiliwa na Polisi waachiwe huru.
Hali hiyo ilijitokeza jana katika Kata ya Hogolo, Tarafa ya Zoisa, wilayani Kongwa. Mkuu wa Wilaya hiyo, Alfred Msovella alisema kuwa waganga hao maarufu kama ‘lambalamba’ walikuwa wakifanya shughuli zisizo rasmi za kuwabaini watu wanaojihusisha na ushirikina.
Alisema walizuiwa na Serikali kufanya shughuli hizo lakini katika hali ya kushangaza wakazi wa kata hiyo wamekuwa wakisisitiza kuwa ni lazima kikundi hicho kiruhusiwe ndipo waweze kuhesabiwa.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema juzi kuwa wakazi hao walifunga barabara kama ishara ya kukataa kuhesabiwa, jambo ambalo lilifanya magari kushindwa kupita.
Alisema kutokana na hali hiyo waliamua kupeleka askari polisi ili kuimarisha usalama lakini hawakumudu jambo ambalo liliwalazimu kuomba nguvu mkoani na walifanikiwa kuletewa askari wa kutuliza ghasia.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya, FFU walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao ambao walikuwa wakisisitiza kuwa hawatahesabiwa hadi hapo waganga hao waachiwe huru.
Msovella alisema juzi hali hiyo ilijirudia baada ya kundi kubwa la vijana kufunga barabara kwa magogo wakipinga kuhesabiwa. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen ambaye alisema pamoja na kutokuwa msemaji wa masuala ya sensa, polisi haiwezi kuwaachia waganga hao kuendelea na shughuli ambazo zilishapigwa marufuku.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Rehema Nchimbi alisema Serikali imepata taarifa hiyo na haiwezi kumwachia mtu yeyote mwenye makosa kwa shinikizo la watu.
Dkt. Nchimbi alisema sensa haina uhusiano wowote na masuala ya ushirikina, hivyo yeyote atakayebainika kuharibu shughuli hiyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, hadi juzi hakuna mtu aliyekuwa anashikiliwa kutokana na tukio hilo.SOURCE WWW.WAVUTI.COM