Saturday, January 31, 2015

TAARIFA MAALUM KUHUSU DENI LA SH. 1,875,896,246,224.48 AMBALO SERIKALI INADAIWA NA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII


2.7.1
​Mheshimiwa Spika, tarehe 24 Oktoba, 2014, Kamati ilifanya kikao cha mashauriano kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gavana wa Benki Kuu, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Msajili wa Hazina na Wakurugenzi Wakuu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

2.7.2
​Mheshimiwa Spika, Dhumuni la kikao hicho lilikuwa kujadili na kutafuta ufumbuzi juu ya hoja ya ukaguzi iliyoibuliwa kwenye Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusiana na ukaguzi kwa Hesabu za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma zinazoishia tarehe 30 Juni 2013. Kwa mujibu wa Taarifa hiyo na ukaguzi uliofanyika baadaye, mpaka kufikia tarehe 30 Septemba 2014 Serikali ilikuwa inadaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii jumla ya Sh.1, 875,896,246,224.48. Aidha, ilifahamika kuwa deni hilo halijumuishi deni la Serikali kwa PSPF la Sh. 7,066,530,000,000.00 ambalo lilianza mwaka 1999 baada ya PSPF kulipa mafao ya Wanachama ambao kisheria walistahili kulipwa lakini walikuwa hawachangii kwenye Mfuko huo.

2.7.3​
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa kulipwa kwanza kwa deni la Sh.1, 875,896,224.48 ili mifuko ya Hifadhi ya Jamii iweze kujiendesha bila matatizo, makubaliano yafuatayo yalifikiwa katika kikao hicho:-

a) Serikali kulipa kwanza asilimia 50 ya deni hilo kwa kutoa Hati fungani (Special Government Bond) ifikapo tarehe 14 Novemba, 2014 endapo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii itasamehe kiasi cha tozo kilichojumuishwa katika deni hilo kinachotokana na malimbikizo ya madeni kwa miradi na mikopo ya Serikali.

b) Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kujadiliana na Bodi za Wadhamini kuhusu kuridhiwa kwa ombi la Serikali la kusamehewa na Mifuko hiyo kiasi cha tozo kilichojumuishwa kwenye deni hilo ili iweze kulipa sehemu ya deni hilo kwa utaratibu ulioelezwa hapo juu.

2.7.4​ 
Mheshimiwa Spika, Bodi za Wadhamini wa Mifuko hiyo ziliridhia kusamehe tozo hizo endapo Serikali ingetoa Hati Fungani hiyo tarehe 14 Novemba, 2014. Lakini cha kusikitisha Serikali haikutimiza ahadi yake na mpaka Kamati inawasilisha taarifa yake makubaliano hayo hayajatekelezwa na Mifuko imeendelea kuwa katika hali mbaya ya kifedha. Kamati inapendekeza kuwa Serikali itekeleze makubaliano hayo mara moja na bila kuchelewa na ukopaji holela wa Serikali kwa Mifuko wa Hifadhi ya Jamii
nchini ukome mara moja.

3.7 ​
Mapendekezo ya kuinusuru Mifuko ya Hifadhi ya Jamii isishindwe kutoa huduma kwa Wanachama wake na Wastaafu kutokana na Serikali kushindwa kuilipa Deni la Jumla ya Sh.1, 875,896,246,224.48.

​KWA KUWA, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inakabiliwa kupungukiwa uwezo wa Fedha za kujiendesha kutokana na Serikali kushindwa kulipa deni la Sh. 1,875,896,246,224.48 kama ilivyoainishwa kwenye Sehemu ya Pili ya Taarifa hii,

​NA KWA KUWA, Kamati imefanya kila linalowezekana kuwezesha deni hilo lilipwe kwa manufaa ya wanachama wa Mifuko hiyo na Wastaafu,

​HIVYO BASI, Kamati inaliomba Bunge lako Tukufu kuazimia Serikali ilipe deni hilo haraka iwezekanavyo ile kuinusuru Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika changamoto ya kushindwa kulipa mafao ya Wastaafu na kutoa huduma nyingine.

Zitto Kabwe

No comments:

Post a Comment