Tuesday, March 25, 2014

SITTA HUU NDIYO WAKATI MUAFAKA...SOAMA ZAIDI HAPA



KAMA inavyokuwa siku zote, siwezi kusema lolote na nyinyi pasipo kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kufika hapa tulipo leo. Yeye ndiye bingwa wa miujiza na hakika kwake, hakuna lisilowezekana.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la katiba, Mh. Samuel John Sitta.

Baada ya kusema hayo, niwashukuru sana Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Jaji Joseph Sinde Warioba kwa hotuba zao nzuri walizozitoa mbele ya Bunge Maalum la Katiba, wakati wa uwasilishwaji wa rasimu na uzinduzi rasmi wa chombo hicho. 

Hakika, lilikuwa ni jambo la kufurahisha sana kuwaona viongozi hao wakitoa hotuba ambazo ziliwavutia sana watu waliozisikiliza, kwani kila mmoja alijenga hoja kwa umahiri wa hali ya juu, kiasi cha wananchi kuzidi kuchanganyikiwa kuhusu mustakabali wa taifa letu, hasa kwa masuala nyeti kama yale yanayohusu muungano wetu. 

Kwa maoni yangu, wote wawili walikuwa na hoja kwa wanachokiamini, kilichobaki ni kuwaachia wajumbe wa Bunge Maalum kuchuja pumba na mchele, ili Mtanzania ale wali safi usio na chenga. 

Hata hivyo, pamoja na wajumbe kuwa na jukumu hilo zito mbele yao, bado hawa hawawezi kufanikiwa kama Mwenyekiti wao, Samuel John Sitta na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan hawatawaongoza kuijadili rasimu hiyo kwa kufuata misingi ya haki, usawa na kuweka mbele masilahi ya nchi, bila kujali itikadi zao za kisiasa. 

Sitta alijijengea heshima kubwa sana wakati akiwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani aliliendesha vizuri, kwa haki na bila upendeleo. Aliruhusu mijadala yenye tija kwa taifa na kamwe hakuitetea serikali bungeni, licha ya ukweli kwamba chama chake ndicho kiliunda serikali. 

Lakini napenda kumweleza mzee Sitta kuwa Bunge la Katiba ni zaidi ya lile alilomwachia mama Anne Makinda. Hili linazungumzia uhai wa taifa letu, siyo tu kwa sisi tulio leo, bali kwa vizazi vyetu vijavyo. Ni bunge la kihistoria na heshima aliyoipata ya kuliongoza, ni tunu ya pekee kwake. 

Ni lazima aelewe, ndani ya Bunge hilo kuna wajumbe kutoka makundi mbalimbali, bila shaka kila moja litataka kuwasilisha na kutetea masilahi yao binafsi, yenye kukidhi matakwa yao. Ni sawa, waache watetee makundi yao. Sisi tunamtaka achuje, aweke mbele kwanza masilahi ya taifa, kama alivyofanya wakati ule akiwa Spika. 

Ni yeye pekee ndiye anayeweza kutuongoza kuelekea kupata katiba tunayoitaka. Rai yangu kwake ni kumtaka kuwa makini kama wengi wanavyomtarajia. Ninajua hata yeye ni mfuasi wa kundi mojawapo linalotaka baadhi ya mambo yao yapitishwe. Ninaomba busara imuongoze kutambua kuwa taifa lina maana zaidi kuliko chama chake cha siasa. 

Aruhusu hoja zitawale, hata kama hazitalipendeza mojawapo ya kundi. Asimamie kanuni vizuri na atoe nafasi hata ya wachache kusikika. Tunajua bunge hili siyo la mwisho kuipitisha katiba mpya, kwa sababu baada ya wao itabidi ipigiwe kura ya maoni na wananchi. Lakini endapo wao wataikosea katika kuijadili na kuipitia, maana yake ni kwamba wananchi watapigia kura katiba mbovu. 

Ikipitishwa katiba mbovu, hii ndiyo itakayokuwa sifa ya Samuel
Sitta, kama mwenyekiti wa bunge hili. Vizazi vijavyo vitawahukumu wajumbe wa bunge hili, hasa aliyewaongoza kupitisha kitu ambacho kitawaletea matatizo badala ya manufaa kama tunavyotarajia.
Kwa hadhi aliyojijengea wakati ule akiwa spika, ni wazi kwamba wananchi wana imani kubwa na utendaji wake na wengine wakaenda mbali zaidi na kudai kuwa anafaa kuwa rais wa nchi. Hatutaki upendeleo, uoga wala hujuma. Hatutaki mtu yeyote atoke ndani ya ukumbi huo baada ya kazi yao kumalizika huku akijitangaza kuwa ameshinda. 

Ikitokea kundi moja kujitangazia ushindi, tujue tumeshindwa kupata katiba bora. Itapendeza siku ya mwisho, watu wote watoke  wakitabasamu kuonyesha wao kama taifa, wameibuka washindi! Lakini wakumbuke pia kuwa wameahidi mbele ya Mungu kuwa watajadili bila upendeleo, atakaekiuka atakuwa amemkufuru Mungu na asubiri mapigo yake.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
-GPL

No comments:

Post a Comment