Friday, January 3, 2014

HUU NDIO UNDANI WA SIRI SIRINI KIFO CHA DOKTA MGIMWA...FUATILIA ZAIDI HAPA...

 



Marehemu Dk. William Mgimwa.
WAKATI taifa likiwa katika msiba kufuatia kifo cha Waziri wa Fedha, Mipango na Uchumi, Dk. William Mgimwa, wananchi wameitaka serikali kueleza kwa nini kwa kipindi chote cha kuumwa kwake, ugonjwa uliomuua ulifanywa siri.

Waziri Mgimwa alifariki dunia Jumatano (juzi) saa 5:20 asubuhi kwa saa za Afrika Kusini (Tanzania saa 6:20) katika Hospitali ya Mediclinic Klooff jijini Johannesburg nchini humo. 

Vyanzo mbalimbali kutoka wizara hiyo vinasema, waziri Mgimwa ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la  Kalenga, Iringa, kabla ya kuugua alikuwa na wakati mgumu kiutendaji kutokana na shinikizo mbalimbali alizokuwa akizipata. 

“Kuna mambo sana pale wizarani, waziri alikuwa na wakati mgumu sana, haya mambo ndiyo yalimfanya hata akajikuta anapata matatizo na kuugua,” kilisema chanzo hicho ambacho kilikataa kutoa ufafanuzi zaidi wa mambo hayo yaliyomtokea kiongozi huyo. 

Ijumaa liliwasiliana na daktari mmoja bingwa wa magonjwa ya binadamu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kuulizwa kama mtu ambaye ana matatizo ya mara kwa mara kazini kwake na kufokewa au kupewa amri anaweza kupata na tatizo gani, akafafanua. 

Akifafanua zaidi, daktari huyo kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini alisema upo uwezekano wa marehemu Mgimwa kuwa alipata ugonjwa unaosababishwa na damu kuganda na kuziba kwenye njia ya mishipa. 

“Kama mnasema alikuwa akipata shinikizo huko kazini kwake, basi huenda alitokewa na kitu kinachoitwa kitaalam Trans Ischaemic Attack (TIA). Hii ni hali ya damu au mafuta kuganda na kuziba kwenye mishipa, hivyo kusababisha damu kushindwa kutembea kuelekea sehemu mbalimbali kwenye mfumo wa ubongo,” alisema daktari huyo na kuongeza: 

“Mara nyingi watu wanaopata tatizo hilo husababishwa na kupewa taarifa za kushtua kama kufokewa au kugombeshwa na kusababisha msongo wa mawazo.” 

Akitoa ufafanuzi zaidi, daktari huyo alisema, TIA huweza kumtokea mtu yeyote na kwamba kwa kawaida, hudumu kati ya dakika moja hadi tano na anayekutwa na hali hiyo, kama asipopatiwa tiba mapema, huwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa kupooza (stroke).
“Lakini kama hali hiyo itaendelea kuwepo pasipo damu au mafuta yaliyoganda kuyeyuka, basi mishipa hushindwa kupitisha damu kuelekea sehemu za ubongo na hivyo kusababisha eneo hilo kufa.

Kadri TIA inavyokaa muda mrefu ndivyo madhara yanavyokuwa makubwa ya kuweza kusababisha kupooza au hata kifo,” alisema.
Hata hivyo, wananchi wameishauri serikali kuweka wazi taarifa za maradhi ya viongozi wa ngazi za kitaifa ili kuondoa sintofahamu mitaani. 

No comments:

Post a Comment