Wednesday, November 13, 2013

WAZIRI AMLAZIMISHA MWANAFUNZI WA MIAKA 14 KUFANYA NAYE NGONO, KWA KUMPA MATUMIZI YA SHULE,, MWANAFUNZI YATIMA,, YADAIWA AMEMUAMBUKIZA UKIMWI,,, SOMA HAPA INASIKITISHA


MMOJA wa mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tatu na mbunge anayetoka Mkoa wa Tabora, anatuhumiwa kumbaka na kisha kutishia kumuua msichana yatima mwenye umri wa miaka 16  anayesoma Shule ya Sekondari Turiani iliyoko Magomeni jijini Dar es Salaam.

Waziri huyo (jina lake linahifadhiwa kwa sasa), ametoa tishio hilo la mauaji kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba iliyosajiliwa kwa jina lake kwa kile alichodai kukaidi amri ya kutaka wasifichue uchafu wake kwa waandishi wa habari.

Akizungumza kwa uchungu na gazeti la  Tanzania Daima, mwanafunzi huyo alisema kuwa waziri huyo  alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo hicho katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012.

Mwanafunzi huyo alisema alifikwa na ukatili huo alipoitwa na kiongozi huyo kwenda kuchukua fedha za ada na matumizi mengine, ambapo mara ya kwanza alimpa sh 700,000 na mara ya pili sh 350,000.

Yatima huyo anayeishi na dada yake, alikutanishwa na waziri huyo wa zamani na baba wa mwanafunzi mwenzake, kutokana na msaada mkubwa aliompa akiwa mgonjwa, ili aweze kumsaidia fedha za ada  kama ishara ya shukurani.

Mwanafunzi huyo alisema baada ya kutambulishwa, aliitwa katika hoteli hiyo ambako baada ya kufika mapokezi wafanyakazi walimkataza kuingia chumbani kutokana na umri wake kuwa mdogo (mwaka 2011 alikuwa na miaka 14), lakini waziri huyo wa zamani aliamrisha aruhusiwe.

Akiwa chumbani, mwanafunzi huyo alilazimishwa kulala naye kisha kumpa sh 700,000, badala ya shilingi 67,000 alizohitaji kwa ajili ya ada.

Mwanafunzi huyo alisema baada ya muhula mmoja aliitwa tena na kiongozi huyo katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012, ambapo pia alimlazimisha kulala naye kwenye zulia la ofisi yake, kisha kumpa sh 350,000.

Mwanafunzi huyo alisimulia kwamba wakati anatoka kwa huzuni ofisini kwa mbunge huyo, mmoja wa wahudumu alimuuliza sababu ya huzuni yake na akalazimika kumweleza kisa hicho, ndipo  mhudumu alitokwa machozi huku akimwambia kwamba, atakufa kwa sababu “baba huyo ni muathirika wa ukimwi”.

Aliongeza kuwa baada ya kuambiwa vile alilia na kufanya fujo hapo mapokezi, hadi alipokamatwa na walinzi, kisha kupelekwa kituo cha polisi kufunguliwa mashitaka.

Hata hivyo, alisema polisi waliposimuliwa kisa chote, walilazimika kumwita waziri huyo wa zamani na alipofika alikiri na kuomba mambo yaishie hapo.

“Alikubali na akaahidi kunilipia ada na pesa za matumizi kiasi cha sh 300,000 kila mwezi, jambo ambalo amekuwa akilitekeleza kupitia simu yake ya mkononi (namba za simu tunazo),” alisema.

Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, Januari 24, mwaka huu walitishiwa maisha na kiongozi huyo, lakini mwezi uliofuata, mtu asiyefahamika alienda nyumbani kwao na kuacha gari (namba tunazo) aina ya Mercedes Benz yenye rangi ya bluu wakati akiwa shuleni, kisha kuacha ufunguo kwa jirani yao kwa maelekezo kuwa akifika apewe.

Wamesema baadaye kiongozi huyo aliwapigia simu kuwaarifu kuwa amempa zawadi ya gari kwa ajili ya matumizi, na wanaruhusiwa kuliuza ili wapate pesa za mahitaji yake siku zilizosalia, kwani baada ya uchaguzi mkuu 2015, atakuwa Waziri Mkuu, hivyo itakuwa ngumu yeye kumtumia huyo binti pesa kama alivyoelekezwa na Jeshi la Polisi kituo cha Oysterbay.

Hata hivyo, wasichana hao walishindwa kulitumia gari hilo hivyo kutoa taarifa polisi ili kesi ipelekwe mahakamani.

Wamedai kuwa polisi walikubali kulipeleka tatizo hilo kwa katibu wa Bunge, ambaye alimwita mwanafunzi huyo na nduguye Dodoma kukutana na Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge.

Hata hivyo, walipofika Dodoma hawakuweza kupata ufumbuzi kwa maelezo kuwa waziri huyo wa zamani hakuwepo hadi Bunge lilipoisha. Kwa muda wote, wasichana hao walisema waligharimiwa kila kitu na Ofisi ya Bunge.

Kabla ya kurudi Dar es Salaam, mabinti hao walisema waliitwa na kiongozi mmoja wa juu wa CCM aliyewalekeza kwenda kumwona Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.

Kwa mujibu wa mawasiliano, kiongozi mwingine (jina tunalo)  alimpigia binti huyo simu majira ya asubuhi, akimtaka aende ofisi za CCM, lakini hakupata msaada wowote zaidi ya kuombwa asubiri hadi wakati wa kipindi cha Bunge ili apate msaada kwa kuwa ni suala binafsi.

Hata hivyo, wakati akiwa njiani kuelekea katika kituo kimoja cha runinga kwa ajili ya kutoa kilio chake, mwanafunzi huyo na dada yake walifuatiliwa na watu wasiowajua, jambo lililowalazimisha kuomba msaada wa wapita njia.

Hata alipofika katika ofisi za kituo hicho cha runinga, watu watatu akiwemo mwanamke mmoja walifika wakidai kuwa ndugu wa wasichana hao na kuwakataza waandishi wasikubali kusikiliza neno lolote, wakati sio kweli.

Aidha, walitumiwa ujumbe kutoka katika namba ya mmoja wa wafanyakazi wa makao makuu ya CCM, akiwasihi kufumba mdomo kwa kuwa anawapenda na hataki wadhurike.

Baada ya jitihada za kuwanyamazisha wasichana hao kushindikana, ndipo mwathirika alipoanza kupokea ujumbe wa kutishia maisha kupitia katika namba ya simu ya 078499…. Ikisema: “Waandishi hawatakusaidia kamwe, Bunge la Katiba likianza watu watakusahau kama uliuawa.

 Mtasahaulika kabisa, subirini mje mzikwe leo usiku kwenu, sitanii, hakuna wa kunifanya lolote, serikali ndio sisi, salini kabisa.”

Jitihada za kumpata waziri huyo wa zamani na mbunge wa CCM, ziligonga mwamba. Mara ya kwanza simu yake moja ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kama dereva wake, na akataka aambiwe sababu za kumuhitaji kiongozi huyo.

Hata aliposisitizwa kuwa anayehitajika ni mkubwa wake, alitoa namba nyingine ya kumpata, lakini ilikuwa ikikatwa mara zote ilipokuwa ikiita.

Mbali ya ujumbe huo wa vitisho, binti huyo alikuwa akitumiwa ujumbe mbalimbali na watu asiowafahamu, na wengine kumpigia simu wakimwambia wanajua amejificha wapi na kwamba hawezi kutoka.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizi nzito, alionyesha kushangaa na kuhoji; “na wewe umeanza kuandika mambo kama haya?”

“Hilo ni jimbo binafsi zaidi na mimi siwezi kuongea lolote,” alisema na akakata simu.

Tanzania Daima Jumatano, liliwasiliana na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, ambaye anadaiwa kulielewa vema suala hilo.

Shelukindo, hata hivyo, licha ya kukubali kuwa alikuwa anajua tatizo hilo, aliomba asiongee kwa kirefu kwa madai kuwa alikuwa kwenye kikao.

Kamanda wa zamani wa polisi Mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela alipulizwa namna alivyoshughulikia jambo hilo, alikana kujua chochote kwa madai kwamba, mambo kama hayo yanashughulikiwa na dawati maalumu.


Credit: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment