Saturday, November 16, 2013

MIKOA KUMI NA SITA YA TANZANIA KUKOSA UMEME KWA SIKU KUMI NA MOJA KUANZIA LEO TAREHE 16

WATEJA katika mikoa inayopata umeme kwenye gridi ya Taifa wanatarajiwa kupata adha ya upungufu wa umeme kwa siku 11 kuanzia leo, kutokana na upungufu wa gesi kutoka katika Kisiwa cha Songosongo kilichopo wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.
 
Hali hiyo imetajwa inatokana na kuwapo kwa matengenezo ya kiufundi kwenye visima vya gesi unaofanywa na Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Limited (PAT).
 
Meneja Uhusiano wa TANESCO, Badra Masoud aliyasema hayo Dar es Salaam jana, akisema upungufu huo utatokea kati ya Novemba 16 hadi Novemba 26, mwaka huu na itahusisha maeneo yaliyopo katika mikoa iliyounganishwa katika gridi ya Taifa.

 
“Tumepata barua kutoka kwa kampuni ya Pan African inayotuuzia gesi, wakisema inafanya matengenezo hayo kuboresha upatikanaji wa gesi ya kutosha kwenye visima hivyo. Uongozi unaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza kwa baadhi ya maeneo yatakayokuwa yakikosa umeme,” alisema.
 
Kwa mujibu wa Masoud, kutokana na matengenezo hayo mikoa iliyounganishwa katika gridi ya Taifa itaathirika kwa kukosa umeme kwa baadhi ya maeneo na kwa nyakati tofauti na kuongeza huduma ya umeme ni muhimu kwa kila Mtanzania kwa ajili ya kujiinua kiuchumi na kipato, lakini matengenezo hayo ni muhimu kwani itaboresha upatikanaji wa gesi kwa ufanisi zaidi.
 
Aliitaja mikoa na maeneo yatakayokumbwa na upungufu wa umeme kuwa ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Dodoma, Morogoro, Singida, Mwanza, Mara, Mbeya, Iringa, Tabora, Shinyanga, Manyara na Zanzibar.
 
Masoud alisema gesi imekuwa ikiwawezesha kutoa Megawati 100 katika kituo cha Ubungo 1, Megawati 100 katika kituo cha Ubungo 2, kituo cha Tegeta Megawati 45 wakati Kampuni ya Songas imekuwa ikitoa Megawati 182 na kuongeza kutokana na matengenezo hayo kutakuwa na upungufu wa Megawati kati ya 150 na 200 na kwamba uzalishaji wa umeme kutumia mafuta na maji utaendelea.
 
Alisisitiza kuwa upungufu huo wa umeme sio mgawo ila ni kupitisha matengenezo ya kiufundi ya Kampuni ya Pan African ambayo alidai kuwa ilishaiomba Tanesco miezi miwili iliyopita ikitaka kufanya matengenezo hayo ambayo hayaepukiki na yenye lengo la kuleta ufanisi zaidi.
 
Masoud alitoa wito kwa wananchi kuwa wavumilivu siku hizo 11 wakati matengenezo yakifanyika na kuwa lengo ni kuboresha upatikanaji wa gesi ya kutosha kwa ajili ya kuzalisha umeme wa kutosha na kutoa huduma inayoridhisha ya nishati ya umeme kwa wateja wake.

-Habari Leo

No comments:

Post a Comment