Sunday, October 20, 2013

WALIOFICHA MABILIONI USWIS SASA KUKUTANA NA MKONO WA SHERIA,TIMU YAPELEKWA KUFANYAKAZI

Taarifa zilizolifikia Mwananchi Jumapili na kuthibitishwa na Zitto jana jioni zilieleza kuwa Eurodad ambao ni mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali 48 kutoka nchi 19 za Ulaya, yanayojihusisha na masuala ya kufuatilia madeni ya nchi zinazoendelea, kwa muda sasa umekuwa ukipambana na watu wanaokwepa kulipa kodi. Picha na Maktaba 
Kwa ufupi
Kazi hiyo ya uchunguzi inaanza leo hadi Novemba 5, mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine watafanya ziara ya uchunguzi kuhusu masuala ya uwazi katika kodi katika nchi za Ulaya.

Dar es Salaam. Wakati ikisubiriwa ripoti ya uchunguzi wa Tume Maalumu iliyoundwa kwa Azimio la Bunge kuchunguza kashfa ya vigogo walioficha Sh323.4 bilioni katika benki nchini Uswisi, Shirika la Kimataifa la Mtandao wa Ulaya wa Madeni na Maendeleo (Eurodad), leo linaanza kuwachunguza walioficha mabilioni hayo ya fedha nchini humo.
Kazi hiyo ya uchunguzi inaanza leo hadi Novemba 5, mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine watafanya ziara ya uchunguzi kuhusu masuala ya uwazi katika kodi katika nchi za Ulaya.
Uchunguzi huo utafanywa na jopo la wataalamu waliobobea katika masuala ya kodi na maendeleo na wataongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema.
Sakata la kashfa hiyo liliibuliwa bungeni kwa hoja binafsi ya Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, mwishoni mwa mwaka 2012.
Zitto alisema kwamba kiasi cha fedha kilichofichwa nchini Uswisi ni kikubwa zaidi ya hicho kilichotajwa.
Kufuatia hoja hiyo, Bunge chini ya Spika Anne Makinda liliipa Serikali kipindi cha mwaka mmoja ambacho kinaishia Oktoba mwaka huu, iwe imekamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti hiyo bungeni.
Ripoti ya Tume hiyo iliyoundwa na Serikali kwa Azimio la Bunge ilitolewa mwishoni mwa mwaka jana, ikiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, mpaka sasa tayari imewahoji vigogo 200 wakiwamo wabunge, wanasiasa na wafanyabiashara.
Muda wa tume hiyo kufanya uchunguzi unakamilika mwezi huu na inatarajiwa katika mkutano ujao wa Bunge unaoanza Oktoba 29 mjini Dodoma, itawasilisha ripoti hiyo.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi Jumapili na kuthibitishwa na Zitto jana jioni zilieleza kuwa Eurodad ambao ni mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali 48 kutoka nchi 19 za Ulaya, yanayojihusisha na masuala ya kufuatilia madeni ya nchi zinazoendelea, kwa muda sasa umekuwa ukipambana na watu wanaokwepa kulipa kodi.
“Mashirika haya yamekuwa kwenye kampeni ya kupinga utoroshwaji wa fedha kupitia ukwepaji kodi unaofanywa na mashirika ya kimataifa kwa nchi zinazoendelea,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa kesho Zitto atakutana na Waziri wa Fedha wa Uswisi na maofisa wa benki mbalimbali na asasi za kiserikali zilizopo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Geneva.
“Zitto pia atahudhuria mkutano wa Kamati ya Kodi ya Umoja wa Mataifa katika kampeni ya kubadili mfumo wa kodi za kimataifa ili kuzuia unyonywaji wa nchi za Kiafrika unaofanywa na kampuni kubwa za kimataifa,” inaeleza taarifa hiyo.
Juzi 21 mwaka huu, Werema alizungumza na Mwananchi Jumapili na kuthibitisha kuhojiwa kwa vigogo hao 200, lakini akasita kuwataja kwa majina kwa maelezo kuwa asingeweza kuwataja kwa kuwa uchunguzi bado ulikuwa unaendelea.
“Uchunguzi huo unaendelea,” alisema Werema huku akisita kueleza kwa undani juu ya kazi hiyo kwa kile alichosema kuwa hana sababu ya kufanya hivyo kwa sasa.
“Subiri uchunguzi bado unafanywa,” alisema Werema na alipotakiwa kueleza utamalizika lini alisema: “Utamalizika tu.”
Uchunguzi wa walioficha mabilioni ya Uswisi uliibuka baada ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB) kutoa taarifa Juni, 2012 kuhusu raia wa kigeni wanaomiliki akaunti za benki nchini humo.
Orodha hiyo iliorodhesha pia baadhi ya Watanzania wenye akaunti zenye fedha zinazofikia Dola196 milioni ambazo ni sawa na Sh323.4 bilioni.
Jarida la kimataifa la uchunguzi la ‘The Indian Ocean Newsletter’ toleo la hivi karibuni, lilimnukuu Werema akisema uchunguzi huo kwa sasa unatia matumaini.
Mbali na Werema, tume hiyo inaundwa na viongozi kadhaa wa taasisi nyeti kama vile Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.
Tume hiyo inawahusisha pia Mkuu wa Sheria wa BoT, Mustapha Ismail na maofisa kutoka idara ya upelelezi na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa jarida hilo la kimataifa, miongoni mwa watuhumiwa hao ni wanasiasa na majenerali wastaafu wanaotuhumiwa kutorosha zaidi ya Dola133 milioni mwaka 2005, kupitia Mfuko wa Ulipaji Madeni ya Nje (EPA)
Baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika wamehojiwa kutokana na taaluma zao, familia zao, akaunti zao za benki zilizoko nchini na nje ya nchi pamoja na nchi walizotembelea mara kwa mara kwa miaka mitatu iliyopita.
Lengo la kuwahoji inaelezwa ni kutaka kujua iwapo walifuata njia zinazotakiwa katika kufungua akaunti hizo nje ya nchi na iwapo fedha zilizohifadhiwa huko zilipatikana kihalali.
Akiwa mkoani Tabora wiki moja iliyopita katika mikutano ya kuimarisha chama, Zitto alisema tayari amemwandikia barua Katibu wa Bunge kutaka taarifa ya uchunguzi huo itolewe katika mkutano ujao.

No comments:

Post a Comment