Tuesday, October 15, 2013

Maiti ya mwanaume yafukuliwa, yakatwa kichwa

Katika hali isiyokuwa ya kawaida wilayani hapa, Mkoa wa Geita, watu wasiojulikana wamefukua kaburi la mtu aliyekufa na kuzikwa katika makaburli ya mtaa wa Elimu Nyantorotoro, kisha kukata kichwa chake na kuondoka nacho kusikojulikana.

Tukio hilo limekuja siku chache wakati wakazi wa Wilaya ya Geita wakiwa na hofu baada ya kutokea tukio la mtoto Shaabani Maulidi (16) aliyefariki miaka zaidi ya miwili iliyopita na kuonekana akiwa hai jirani na mtaa huo.

Katika tukio hilo ambalo limekusanya umati mkubwa wa wakazi wa mji wa Geita, lilitokea jana baada ya watu kukuta jeneza la maiti likiwa limefukuliwa na kupasuliwa na baadae kutoa kichwa cha maiti hiyo ya mwanaume (jina halijafahamika), kisha kuondoka nacho na kuliacha kaburi likiwa wazi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Elimu Nyankumbu, Hassan Malima, alisema tukio hilo liligunduliwa saa tatu asubuhi na watu walioenda eneo hilo kuchimba kaburi baada ya kutokea msiba kwa mchungaji Mtafuteni Mihana, wa kanisa la Pefa, aliyefiwa na mtoto wake.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, maiti hiyo ilizikwa takribani miezi mitatu iliyopita.

Hata hivyo, ndugu na jamaa wa karibu wa marehemu huyo hawakupatikana haraka kuzungumzia tukio hilo.

Malima alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo linalohusishwa na imani za kishirikina, walitoa taarifa polisi ambao walifika haraka katika eneo hilo wakiongozwa na mkuu wa polisi wilaya ya Geita, OCDBwire.

Baada ya kufanyika uchunguzi wa kitabibu uliofanywa na Dk. Alex Makonda, alibainisha kuwa marehemu huyo alikuwa ni mwanaume.

Naye mchungaji wa kanisa la Pefa, katika mtaa huo, Mchungaji Mtafuteni alisema tukio hilo limetokana na imani za kishirikina na kwamba imesababishwa na watu kukosa hofu ya Mungu.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment