WILAYA ya Kishapu mkoani
Shinyanga imetajwa kuwa inaongoza kwa tatizo la utapiamlo kwa watoto miongoni
mwa wilaya 40 nchini, ambazo hivi karibuni zilifanyiwa tathmini ya hali ya
chakula na lishe.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na
Ofisa Lishe wa Mkoa wa Shinyanga, Mariam Mwita, tathmini ya hali ya chakula
iliyofanywa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Septemba, 2012
katika wilaya 40 nchini matokeo yalionesha wilaya ya Kishapu ilikuwa na hali
mbaya zaidi.
Akitoa taarifa hiyo mkoani Shinyanga, Mwita alisema mbali ya
wilaya hiyo pia wilaya ya Shinyanga ilikuwa hatarini baada ya asilimia kubwa ya
watoto waliopimwa kubainika wana utapiamlo.
Alisema takwimu za upimaji huo zilionesha asilimia 43 ya watoto
waliopimwa walikuwa wamedumaa, asilimia 10 walikuwa na uzito pungufu, upungufu
wa damu walikuwa ni asilimia 75, uhaba wa madini chuma asilimia 48.
Asilimia tatu ya watoto walikuwa wamekonda huku asilimia 37 wakiwa
na tatizo la upungufu wa vitamini A.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Wilson Nkhambaku,
alielezea kushutushwa kwake na takwimu hizo na kwamba inampa uchungu hasa pale
anapokumbuka kuwa wilaya hiyo ni moja ya wilaya ambazo halmashauri zake
zilitajwa pia na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwa na hesabu chafu.
Kutokana na hali hiyo
mkuu huyo ameyaomba mashirika mbalimbali ya umma na ya kibinafsi ikiwemo
Shirika la World Vision kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wakazi wa wilaya hiyo
ili kuwapatia chakula kitakachoweza kuwasaidia kuboresha lishe zao.
Akizungumzia hali hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga, aliwaomba wajumbe wa kamati ya lishe
ya mkoa iliyoundwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali kuhakikisha wanafikisha
elimu ya lishe bora kwa wananchi hasa walioko maeneo ya vijijini.
Mkuu huyo aliwaomba
wakazi wa mkoa wa Shinyanga kuhakikisha wanazingatia ushauri wa mara kwa mara
unaotolewa na wataalam wa afya na wajitahidi kutunza afya zao vizuri ikiwemo
suala la kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara.
“Tatizo la utapiamlo linatibika, ni muhimu tukazingatia ushauri wa
wataalamu wa afya, tule vyakula vyenye lishe, tufanye mazoezi angalau muda wa
nusu saa kila siku, tule milo kamili hasa kwa kuzidisha ulaji wa mboga za
majani na matunda,” alisema Rufunga.
No comments:
Post a Comment