Mzozo wa wapenzi wawili usiku, umesababisha mmoja wa kike kupiga mayowe
ya kumuita mwenzake mwizi, akavamiwa na watu waliompiga na kumchoma moto
hadi kufa.
Kisa hicho kimetokea mkazi wa Magazini mjini Mpanda mkoani Katavi,
Florence Mabuga (29), ambaye baada ya kuvamiwa na watu akidhaniwa mwizi,
alipigwa na kuuawa na mwili wake kuchomwa moto mbele ya nyumba yake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, amethibitisha
kuuawa kwa mkazi huyo katika kisa hicho kilichotokea katika mtaa wa
Nsemulwa-Magazini hivi karibini, usiku wakati Mabuga akimsindikiza
mpenzi wake wa kike akitokea nyumbani kwake.
Akisimulia mkasa huo wa kusikitisha, Kamanda Kidavashari alisema
Mabuga ambaye alikuwa msimamizi wa vibarua wa kujenga nyumba mjini
humo, siku hiyo baada ya kurejea nyumbani, alitembelewa na mpenzi huyo
ambaye jina lake halijafahamika.
Inadaiwa wakati Mabuga akimsindikiza rafiki huyo, ulizuka mzozo baina
yao ambapo Mabuga alitishia kuwa usiku huo angechoma nyumba ya
rafiki huyo, ndipo kwa hasira na hofu ya kuchomewa nyumba, alipiga
yowe akiashiria kuwa Mabuga ni mwizi.
Kwa mujibu wa Kidavashari, Mabuga alianza kutimua mbio mara alipoona
kundi la wananachi wenye hasira wakiwa na silaha mbalimbali za
jadi wakikimbilia alipokuwa amesimama na rafiki yake huyo.
“Uchunguzi wa awali wa kipolisi umebaini kuwa Mabuga alisingiziwa tu
na mpenzi wake huyo, kwani hakuiba kitu chochote, ila mpenzi
wake huyo alimpigia mayowe ya mwizi baada ya kuzuka mzozo baina
yao,“ alidai.
Kwa mujibu wa Kidavashari mtuhumiwa huyo anaendelea kusakwa ili sheria
ichukua mkondo wake, pia hakuna mtu yeyote aliyekamatwa hadi sasa
kwani wananchi hao walikimbia eneo la tukio mara baada ya kufanya
unyama huo.
No comments:
Post a Comment