Wakati walimu wawili wa kujitolea, raia wa Uingereza, wakijeruhiwa kwa
kumwagiwa tindikali, katika maeneo ya Mji Mkongwe, Shangani, Zanzibar,
mapya yameibuka kuhusu walimu hao.
Kate Gee (18) na Kristie Trup (18), walivamiwa na kujeruhiwa juzi saa moja usiku, wakienda kupata chakula cha jioni.
Habari
za kuaminika zilizopatikana jana jioni zinadai kuwa mmoja wa walimu hao
alishawahi kushambuliwa wakati akiwa kisiwani humo wiki mbili
zilizopita.
Kwa mujibu wa mmoja wa marafiki zao, Oli Cohen,
mwenye miaka 21, alisema: "Katie alishambuliwa wiki mbili zilizopita na
mwanamke mmoja wa Kiislamu kwa kuimba wakati wa Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani.
"Alishitushwa mno na tukio hilo - lakini hakupatwa na
hofu kiasi cha kufikiria kurejea nyumbani. Akaendelea kuishi hapo
kumalizia safari yake na kazi yake ya kujitolea."
Akizungumza nje
ya hekalu ambalo Kirstie anaishi na baba yake Marc na mama Rochelle,
rafiki mwingine aliongeza: "Wamemaliza mchezo kwa sasa, inatia wasiwasi
kiasi kuhusiana na kampuni ya bima na balozi mdogo.
Naibu
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Yusuf Ilembo, alithibitisha jana
wasichana hao kujeruhiwa kwa tindikali hiyo, na kusema ni sehemu ya
vitendo vya aina hiyo ya uhalifu vinavyoendelea Zanzibar.
"Tulipata taarifa ya tukio hilo jioni baada ya watu kumaliza kufuturu eneo la Shangani mjini hapa," alisema Kamanda Ilembo.
Taarifa
zilizotufikia jana baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Aga Khan,
Dar es Salaam, zilieleza kuwa wasichana hao walikwenda Zanzibar
kujitolea kufundisha kwa wiki tatu na juzi walikuwa katika wiki ya pili.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, wakati walimu hao wakienda kupata chakula cha
jioni, pikipiki aina ya Vespa, ilisimama mbele yao ikiwa na vijana
wawili, mmoja wao aliwamwagia tindikali walimu hao.
Mwalimu Kate
kwa mujibu wa taarifa hizo, alimwagiwa kifuani na mkononi huku Mwalimu
Kristie akimwagiwa usoni na hali yake ilielezwa kuwa mbaya.
Kristie anatokea Hampstead na Kate ni mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Francis Holland mjini Chelsea.
Mama wa Kate, Nicky alisema familia hizo zinapambana kuwarejesha wanawake hao wawili nyumbani haraka iwezekanavyo.
Wachunguzi
wanasema kundi la Waislamu ambao wanataka Zanzibar ijitenge kutoka
Tanzania wanawezekana kuhusika na shambulio hilo lakini hakuna yeyote
mpaka sasa aliyedai kuhusika na shambulio hilo.
Polisi imeanza uchunguzi wa tukio hilo, kwa nia ya kuwatia mikononi wahusika na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Matukio
ya watu kumwagiwa tindikali ambayo sasa yanaonekana kuelekezwa kwa
wageni, yanaweza kuathiri sekta ya utalii na sasa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar (SMZ) imepanga kujitanua zaidi kupitia masoko ya Asia na
Ulaya.
Wiki iliyopita, wakati Kamishna Mkuu wa Polisi Zanzibar,
Mussa Ali Mussa, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
Ziwani, alisema watuhumiwa wa shambulio la tindikali kama hilo dhidi ya
Katibu wa Mufti, Shekhe Fadhil Soraga na Sheha wa Tomondo, Omar Mohamed
Kidevu hadi sasa hawajakamatwa.
Mwenyekiti wa Chama cha
Wawekezaji kwenye Utalii Zanzibar (ZATI), Abdul Samad, aliliambia
Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), kwamba shambulio hilo linaweza
kuathiri sekta hiyo Zanzibar.
Sekta ya utalii Zanzibar huchangia pato la Taifa kwa asilimia 50, huku ikichangia ajira kwa wananchi kwa asilimia 45.
Watalii kutoka Uingereza wanashika nafasi ya tatu kwa wingi Zanzibar kwa asilimia 20, wakiongozwa na Italia na Afrika Kusini.
Eneo
la Mji Mkongwe linaongoza kwa kutembelewa na watalii wengi kujionea
maeneo ya kihistoria na majengo ya kale kama Kanisa la Anglikana
lililojengwa mwaka 1873 Mkunazini, ambalo ni kichocheo cha kuondoshwa
kwa biashara ya utumwa mwaka 1907.
Rais Jakaya Kikwete alifika
katika Hospitali ya Aga Khan jana mchana, ambapo alikwenda moja kwa moja
katika chumba walimolazwa wasichana hao na kuzungumza nao na kupata
taarifa ya maendeleo yao.
Baada ya hapo, alipita katika chumba alimolazwa Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo na kumjulia hali na kuzungumza naye.
Akizungumza
na waandishi wa habari nje ya hospitali hiyo, Rais Kikwete alisema
uvamizi huo ni wa kusikitisha na kushukuru uongozi wa hospitali hiyo kwa
kuwahudumia vizuri wagonjwa hao.
Rais alisema ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama, kusaka wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Kiongozi
wa Shirika la Art in Tanzania, lililoleta walimu hao nchini, Bashir
Ismail, alisema inaonekana shambulio hilo lililenga walimu hao kutokana
na aina ya mavazi waliyovaa.
Baada ya uvamizi huo, alisema
waliwasiliana na Ubalozi wa Uingereza nchini, ambao ulipeleka ndege
maalumu ikawasafirisha hadi Dar es Salaam ambako waliwasili hospitalini
saa nne usiku.
Alisema katika eneo la tukio, kulikuwa na wageni wengi lakini waliomwagiwa tindikali hiyo ni walimu hao ambao walivaa suruali.
Kuhusu
hali yao ya afya, Ismail alisema pamoja na majeraha, lakini wote
wanazungumza na wakati wowote wakipata ndege, watasafirishwa kurejea
kurudi nchini mwao Uingereza kwa matibabu zaidi.
Hivi karibuni
mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa maduka ya Home Shopping Center
(HSC), Said Mohamed Saad, alimwagiwa tindikali maeneo ya Msasani City
Mall, Dar es Salaam na sasa yuko Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
Alimwagiwa
saa moja usiku, na mtu ambaye hakufahamika na mara baada ya tukio hilo,
mhusika alikimbia huku mlinzi wa eneo hilo akijaribu kumkimbiza bila
mafanikio baada ya kuteleza na kuanguka. Hatua hiyo ilitoa mwanya kwa
mtuhumiwa kutoroka eneo la tukio kwa pikipiki.
Tukio hilo
lilikuja takribani wiki mbili tangu Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Arumeru,
mkoani Arusha, Said Makamba kujeruhiwa usoni kwa kumwagiwa tindikali
usiku akiwa nyumbani kwake.
No comments:
Post a Comment