CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kitendo cha polisi nchini kuendelea kuwapiga wananchi risasi ni matokeo ya taifa kuongozwa na Katiba mbaya. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Willbrod Slaa alikuwa akizungumza katika viwanja vya kituo cha mabasi cha Kilombero wakati wa mkutano wa kukusanya maoni ya kuunda Katiba mpya kutoka kwa wananchi.
Dk. Slaa aliyezungumza kabla ya kuanza kupokea maoni ya wananchi hao, alisema vitendo vingi vinavyofanyika hivi sasa vinafanywa kwa kukiuka misingi na haki za binadamu kutokana na kuwa na Katiba mbaya.
Alikitaka Chama cha Mapinduzi (CCM) kuacha kile alichokiita kuwaburuza wananchi juu ya kutoa maoni yao kuhusu Katiba wanayoitaka.
“CCM acheni kuwaburuza wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Katiba inayotengenezwa hivi sasa si kwa ajili ya CHADEMA wala Kikwete, Katiba inayotengenezwa sasa ni mali ya wananchi.
“Mkijaribu kuvuruga Katiba ili kutoa mianya ya watu kula, nawaambieni hata mkijaribu kwenda misikitini au makanisani kuomba kamwe haitawezekana kupatikana amani.
“Na hivi vitendo vya polisi kuendelea kupiga watu kwa risasi za moto hayo yote ni matokeo ya kuwa na Katiba mbaya,” alisema Dk. Slaa.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo walipendekeza muundo wa Serikali tatu.
Pia walipendekeza kuwapo na uwazi kwenye mishahara ya watumishi wa Serikali na umma ikiwamo kwa Rais mwenyewe.
Wananchi hao walipendekeza Katiba mpya itamke kuwa Kiswahili iwe lugha ya taifa, wakati Kiingereza ikitamkwa na Katiba Mpya kuwa ni lugha ya lazima kufundishia.
Naye Mwanasheria Mwandamizi Mabere Marando, aliwahakikishia wananchi kuwa maoni waliyotoa yatafikishwa mbele ya Tume ya Jaji Joseph Warioba.
No comments:
Post a Comment