Ni nyumba namba 8,115. Ipo ndani ya Mtaa wa Vilakazi, magharibi mwa mji wa Soweto.
Pengine fundi aliyeijenga nyumba hiyo hakufahamu
kuwa siku moja nyumba hiyo ingebeba historia nzito ya kiongozi mashuhuri
duniani, Nelson Mandela.
Ni nyumba ya kawaida pengine ya hadhi ya chini kama zilivyo nyumba nyingi za Tanzania.
Imejengwa kwa matofali ya kuchoma ikiwa na vyumba
viwili vya kulala, sebule ndogo, jiko, pamoja na choo na bafu ambavyo
vipo uwani.
Mbele ya nyumba hii kuna kibaraza kidogo pamoja na bustani ya wastani ambayo katikati ina mti wa kihistoria.
Ni mti wa kihistoria kwani kwa mila za Xhosa,
vitovu vya watoto wachanga huzikwa chini ya mti. Hivyo basi vitovu vya
watoto watatu wa Mandela, yaani Zindzi, Makhaziwe na Lekghato lewanika
Mandela vilizikwa chini ya mti huu.
Baadhi ya samani zilizotumiwa na Mandela pamoja na
familia yake, bado zipo. Kuna kitanda kilichotumiwa na binti zake
wawili, Zindzi na Makhaziwe, kuna jiko la kuni ambalo nalo lilitumiwa na
Winnie kupikia.
Pia zipo pea mbili za viatu vya kijeshi vya Mandela ambavyo alivivaa alipokuwa akilitumikia jeshi la wananchi wa Afrika Kusini.
Kuna kofia kadhaa, picha zake kabla ya kifungo,
mkanda wake wa ndondi na tuzo nyingi zilizosheheni katika kabati kubwa
ambalo sasa limewekwa katika kile kilichokuwa chumba cha kulala cha
Zindzi na Makhaziwe.
Nyumba hii ilijengwa mwaka 1945, ikiwa sehemu ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya watu wa jiji la Johannesburg.
Tsonane Skhumbuzo ni miongoni mwa wafanyakazi katika nyumba hii ambayo kwa sasa ni Makumbusho ya Taifa hapa Soweto.
Anasema, mara baada ya Mandela kuchaguliwa kuwa
Rais wa Afrika Kusini mwaka 1994, aliikabidhi nyumba hii kwa serikali
ili iwe sehemu ya makumbusho.
No comments:
Post a Comment