Tuesday, August 27, 2013

HIVI HUYU MASSAWE NI NANI MBONA HAKAMATWI

                                                                Alex Siliyamala Massawe.

KUNA taarifa za mfanyabiashara maarufu Alex Siliyamala Massawe aliyetimkia nje ya nchi kwa kipindi kirefu sasa huku akisakwa na polisi kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya mauaji, kukamatwa Dubai lakini hajaletwa nchini kujibu mashitaka hayo hivyo kuzua swali zito.

Tayari mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jijini Dar es Salaam chini ya Hakimu Gene Dudu wiki iliyopita imetoa hati ya kukamatwa na kurejeshwa nchini kwa Massawe ili aje kukabiliana na kesi zake mbili ikiwemo ya madai ya kughushi nyaraka mbalimbali.
Hati hiyo ilitolewa baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka kuwasilisha ombi la kutaka mfanyabiashara huyo arejeshwe nchini kwa kuwa tayari amefunguliwa kesi namba 150/2013  ya kughushi na kutoa nyaraka za uongo, hali iliyofanya wananchi kadhaa kuanza kuhoji; Massawe ni nani hadi serikali ishindwe kumkamata na kumleta nchini?
Wananchi hao ambao waliomba majina yao yasiandikwe gazetini walisema wanashangazwa kuona mfanyabiashara huyo anashindikana kukamatwa na kuletwa nchini licha ya kuripotiwa kuwa ametiwa mbaroni na Polisi wa Kimataifa (Interpol) huko Dubai.

IGP Mwema.

“Kwani kuna tatizo gani mpaka serikali inashindwa kumleta nchini? Ni siku nyingi tunaambiwa amekamatwa Dubai, kinachosababisha asiletwe nchini ni nini?” alihoji mwananchi mmoja nje ya mahakama ya Kisutu.
Gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, SSP Advera Senso na alipoulizwa ni lini Massawe atarejeshwa nchini alisema hajui chochote.
“Mimi sijui chochote kuhusu kukamatwa na kuletwa nchini kwa Massawe,” alisema Senso alipoulizwa ofisini kwake.
Licha ya kubabiliwa na kesi hiyo inayohusu nyaraka, Massawe amejumuishwa katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Onesphory Kituli aliyeuawa kwa kupigwa risasi Oktoba 11, 2011 nyumbani kwake Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam ambapo Marijani Msofe ‘Papa Msofe’ na Makongoro Nyerere nao wanahusishwa na  wanashikiliwa na polisi na wapo rumande.

No comments:

Post a Comment