Thursday, June 13, 2013

RAIS JACOB ZUMA ASEMA KUWA AFYA YA NELSON MANDELA YAANZA KUIMARIKA


Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema kuwa afya ya rais wa zamani wa taifa hilo Nelson Mandela imeanza kuimarika kidogo kutokana na matibabu anayopewa na Madaktari wake jijini Pretoria.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela kulia na rais wa sasa Jacob Zuma

Zuma amewaambia wabunge kuwa Mandela anayefahamika kwa jina maarufu kama Madiba ameanza kuimarika na ni habari njema kwa raia wa nchi hiyo ambao wamekuwa wakikumbwa na wasiwasi kutokana na afya yake kuendelea kudorora.

Rais huyo ameongeza kuwa kila mmoja anakumbuka mchango wa Mandela ambaye alifungwa jela miaka 27 akiwa katika harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo na baadaye kufanikiwa kuwa kiongozi wa kwanza mweusi nchini humo mwaka 1994.

Kiongozi huyo wa Afrika Kusini amewataka raia wa nchi hiyo na dunia nzima kuendelea kumwombea Mandela ili apate nafuu haraka na kuruhisiwa kurudi nyumbani.

Familia ya Mandela imesema kuwa imeguswa mno na salamu za heri njema zinazotumwa na watu mbalimbali duniani kumtakia kiongozi huyo wa zamani nafuu ya haraka.

Mandela mwenye umri wa miaka 94 alilazwa hospitalini Jumamosi iliyopita baada ya kuanza kusumbuliwa na mapafu tatizo ambalo limemsumbua kwa muda mrefu.

Hii ni mara ya nne kuanzia mwezi Desemba mwaka uliopita kwa Mandela ambaye atatimiza miaka 95 mwezi ujao kulazwa hospitalini na mara ya mwisho ilikuwa mwezi Aprili mwaka huu.

Mara ya mwisho kwa Mandela kuonekana hadharini ilikuwa mwezi Julai mwaka 2010 wakati wa ufunguzi wa mashindano ya soka ya kombe la dunia nchini humo.

No comments:

Post a Comment