Monday, June 10, 2013

MBUNGE WA MTWARA ASOMEWA SHITAKA LA UCHOCHEZI NA KUREJESHWA RUMANDE BAADA YA KUKOSA DHAMANA


Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnein Murji (kushoto) akiingia katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara jana kusomewa shtaka la kufanya uchochezi. (picha: Haika Kimaro/MWANANCHI)
Mbunge wa jimbo la Mtwara Mjini (CCM), eneo ambalo limekumbwa na vurugu hivi karibuni kusini mwa Tanzania, Hasnein Murji na watuhumiwa wengine 91 wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani humo Jumatatu, Juni 10, 2013 akituhumiwa kwa makosa ya uchochezi wa vurugu zilizosababisha vifo vya watu watatu mwezi uliopita.

Murji amepandishwa kizimbani ikiwa ni moja ya mkakati wa vyombo vya dola kuwasaka na kuwafungulia mashitaka watu inaowatuhumu kuhusika kuchochea vurugu ambazo chanzo chake ni kupinga ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

Mwendesha Mashtaka ambaye ni Wakili wa Serikali, Zuberi Mkakatu aliieleza Mahakama kuwa mnamo Januari 19, mwaka huu, maeneo ya Ligula mkoani hapa mtuhumiwa alichochea watu kutenda makosa.

Washitakiwa wengine 91 waliofikishwa tena mahakamani hapo waliendelea na kesi inayowakabili ya 


uchochezi, uharibifu wa mali kwa makusudi pamoja na kufanya mkusanyiko usiokuwa halali.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mtwara, Dynes Lyimo alisema dhamana iko wazi kwa washitakiwa ambao wana masharti tofaotu yaliyogawanywa kwa mahakimu watatu. Masharti matatu yaliyomkabili Murji ni:
  1. Kuwasilisha hati ya kusafiria mahakamani.
  2. Kuwa na mdhamini mmoja mkazi wa Mtwara ambaye atasaini mali isiyohamishika isiyopungua Sh20 milioni. 
  3. Mshitakiwa kutoruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara pasipo kibali cha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara.

Baada ya kusomewa shitaka na masharti ya dhamana, baadhi ya washitakiwa walipata dhamana na kutoka, wengine wakiendelea na taratibu za kukamilisha udhamini il hali Murji na baadhi ya watuhumiwa walirudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Sharti lililomshinda Murji ni la kukosa pasi ya kusafiria, ambayo aliiacha Dar es Salaam, alikokamatwa.

Mbunge huyo anayewakilishwa na Wakili Chaula Msechu alifikishwa mahakamani hapo jana saa 3.15 asubuhi akiwa katika gari la polisi huku ulinzi ukiwa umeimarishwa. Polisi waliokuwa na silaha na wengine wakiwa na mbwa walikuwa wametanda mahakamani.

Mbali ya mahakamani, polisi walikuwa wakipita katika barabara mbalimbali za Mtwara sambamba na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Licha ya matangazo mbalimbali ya polisi kwamba hakutakuwa na tishio la uvunjifu wa amani, baadhi ya wananchi waliogopa kufungua biashara zao na wengine wakikimbia mji.

Wananchi waliofika mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi zinazowakabili ndugu na jamaa zao wamelalamikia utaratibu wa kuwazuia kuingia mahakamani hapo.

Murji alikamatwa na kushikiliwa na jeshi la Polisi mkoani humo siku ya Jumamosi.

Idadi kubwa ya wananchi wa Mtwara wamekuwa katika mvutano mkali na Serikali ya Tanzania ambayo imekusudia kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia inayopatikana mkoani humo hadi Dar es Salaam , Hatua inayopingwa na wananchi hao ambao wanadai gesi hiyo isisafirishwe na kupelekwa popote.

---

No comments:

Post a Comment