KATIKA hali isiyo ya kawaida na inayoashiria uzembe katika ulinzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, juzi kijana mmoja mkazi wa eneo la Phillips katika Kata ya Sekei jijini Arusha, Hamad Rashid (32) aliiba kiti (kigoda) cha kukalishia Mwenge.
Kuibwa kwa kiti hicho kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas. Kiti hicho hutumika kuwekea Mwenge wa Uhuru unapokuwa katika mbio zake nchi mzima.
Tukio la kuibwa na kisha kukamatwa kwa mtuhumiwa lilitokea juzi saa 11 jioni Sanawari eneo la Mataa. Eneo hilo ndilo lilipangwa kwa ajili ya mkesha wa Mwenge huo baada ya kukamilisha mbio zake na kazi ya kuweka mawe ya msingi na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jiji la Arusha.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Sabas aliyetafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia tukio hilo, alikiri kutokea kwa wizi huo na kuongeza kuwa mtuhumiwa huyo alishakamatwa na polisi waliokuwa wakiulinda Mwenge pamoja na kiti hicho.
Alisema tukio hilo lilitokea wakati Mwenge huo pamoja na wakimbizaji wake kitaifa, kimkoa na viongozi wengine wakiwa katika harakati za kusoma salamu za utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya ratiba ya utangazaji wa ratiba ya mkesha kutolewa.
Alisema kabla ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, alionekana kwa muda mrefu akiwa amesogelea gari lililokuwa limebeba kiti hicho kilichoelezwa na kamanda kuwa kilikuwa cha akiba.
Alisema mara baada ya wizi kijana huyo alikamatwa na katika mahojiano alisema alikuwa anataka kukiangalia tu na kwamba haikuwa nia yake kukiiba na kuomba msamaha.
Hata hivyo alisema polisi wanaendelea kumhoji ili kubaini dhamira halisi ya kukichukua kiti hicho.
Alisema mara baada ya upelelezi wa kesi hiyo, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani ili kujibu mashitaka yanayomkabili ya wizi wa kiti hicho cha Mwenge wa Uhuru.
Mwenge huo wa Uhuru uliingia Arusha Juni 3 mwaka huu ukitokea mkoani Manyara na utakimbizwa katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Arusha kabla ya kukabidhiwa kwa mkoa wa Mara Juni 11, yaani Jumanne ijayo.
No comments:
Post a Comment