WANANCHI wa kijiji cha Mapogolo Kapunga kata ya Itamboleo Wilaya ya Mbarali mkoani hapa wamekataa kupokea majengo ya Shule yaMsingi iliyojengwa na Mwekezaji wa Shamba la Kapunga Rice Project kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri.
Wakizungumza katika Mkutano wa hadhara kijijini hapo baada ya Mwenyekiti wa kijiji hicho Ndugu Ramadhani Nyoni kutoa taarifa Kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Gulam Husein Kiffu juu ya kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo iliyojengwa na Mwekezaji Kilomita 8 kutoka katika makazi ya watu.
Kutokana na kukamilika kwa majengo hayo Mkuu wa Wilaya kupitia Mkutano alioufanya Aprili 25 na Serikali ya Kijiji aliwasihi wananchi kuipokea Shule hiyo ikiwa ni pamoja na kuwahamisha wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Msingi Kapunga na kuhamia Katika shule mpya ifikapo Mei 3 Mwaka huu.
Lengo la kujengewa shule nyingine ni kutokana na Mwekezaji kutaka Wananchi wampishe katika eneo lake hivyo akalazimika kujenga Shule nyingine ambayo baada ya kukamilika Wananchi wameikataa kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri kati ya Mwekezaji na Wananchi wanaoyazunguka mashamba.
Aidha wakizungumzia sababu za kukataa kupokea Majengo hayo Viongozi wa Serikali ya Kijiji wamesema tangu ujenzi uanze hawajawahi kupewa taarifa ya aina yoyote, pia umbali mrefu kutoka maeneo wanayoishi na Shule mpya ilipojengwa ambao ni Kilomita Nane.
Sababu nyingine wamedai kutokuwa na imani na Mwekezaji huyo kutokana na kuwa na tabia ya kuwanyanyasa Walimu ambao awali amewahi kuwafukuza katika majengo ya Shule hali iliyopelekea Walimu hao kutembea umbali mrefu kwenda Shuleni kufundisha.
Akitoa taarifa kwa wananchi katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Aprili 29, Mwaka huu Ofisa Mtendaji wa Kijiji Ndugu Peter Kita amesema Mwekezaji alitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya kuhusu kukamilika kwa ujenzi na kuomba kuwakabidhi ili waanze kuyatumia lakini Wananchi hawakukubaliana naye.
Wananchi hao wamefafanua kuwa wao hawako tayari kupokea majengo ya shule hiyo kutokana na Mwekezaji kutokuwa na msaada wowote katika kijiji ikiwemo Shughuli za Kijamii kama Maji , Afya, Barabara na Umeme.
Wamesema kwa sasa wako tayari kujenga Shule yao kwa nguvu zao ambapo walisema tayari wameshapata kibali na michoro kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Mbarali.
Wameongeza kuwa sababu zingine za kukataa mradi huo ni kuhofia usalama wa wanafunzi kutokana na kuwepo kwa mfereji mkubwa wa maji karibu na Shule ilipojengwa pamoja na ubora wa majengo kuwa hayataweza kuhimili vishindo vya wanafunzi zaidi ya 700.
Mbali na Ajenda ya Shule wanakijiji hao pia walikuwa wakisomewa taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji ambapo pia waliidhinisha bajeti ya kipindi cha Mwaka 2013/2014 zaidi ya Shilingi Milioni 130 zitakazokusanywa kutokana na vyanzo mbali mbali.
Mikakati ya ujenzi wa Shule yao mpya ulianza hapo hapo ambapo zaidi ya Shilingi 90,000/= zilikusanywa na kuazimia kila kaya kuchangia Shilingi 20,000/= hadi ifikapo Mei 15, Mwaka huu ambapo wanatarajiwa kukusanya zaidi ya Milioni Kumi.
Aidha wametoa wito kwa mwekezaji kutowasumbua wanafunzi wanaosoma darasa la nne na darasa la saba kutokana na kuwa na mitihani ya kitaifa ambapo walisema Shule yao mpya inatarajiwa kukamilika katika muda mfupi baada ya kukamilisha maandalizi yote.
Haya hivyo ikumbukwe kuwa Mwekezaji huyo wa Kapunga Rice Project bado anakesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya akituhumiwa kuteketeza mazao ya wananchi kwa sumu na kuwasababishia hasara na madhara wananchi.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment