Wednesday, May 1, 2013

UPELELEZI WA KESI YA LWAKATARE NA LUDOVICK UMEKAMILIKA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya tuhuma za ugaidi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph, ulieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Mbele ya Hakimu Mkazi Alocye Katemana, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Peter Mahugo alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba  kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na hakimu Katemana aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 13  kwa ajili ya kutajwa.

  1. Machi 20 mwaka huu, ilidaiwa mawakili wa serikali  waandamizi Ponsian Lukosi, Prudence Rweyongeza na Peter Mahugo, kuwa kosa la kwanza ambalo linawakabii washitakiwa wote kuwa ni lakula njama kutenda kosa la jinai kinyume na kifungu cha 284  cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , na kwamba mnamo Desemba 28 mwaka jana, huko Kimara King’ong’o  Stopover, wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka kutumia sumu kwa lengo la kumdhuru  Denis Msaki ambaye ni Mhariri wa habari wa Gazeti la Mwananchi, kosa ambalo ni kinyume na kifungu cha 227 cha sheria hiyo.

  2. Wakili Rweyongeza alilitaja  kosa la pili kuwa ni la kula njama  ambalo pia ni kwa ajili ya washitakiwa wote  ambalo ni kinyume na kifungu cha 24(2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi Na.21 ya mwaka 2002, ambapo washitakiwa hao walitenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka Denis Msaki  kinyume na kifungu  cha 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

  3. Shitaka la tatu ni la washitakiwa wote ambapo wanashitakiwa kwa kosa la  kupanga kufanya makosa ya ugaidi  kinyume na kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi kwamba Desemba 28 mwaka jana, walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyara Denis Msaki  kinyume na kifungu 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi.

  4. Shitaka la nne, Rweyongeza alidai kosao linamkabili Lwakatare peke yake kwa kuwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume na kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi, kwamba Desemba 28 mwaka jana, Lwakatare akiwa ni mmiliki nyumba hiyo ilipo Kimaraka King’ong’o  kwa makusudi aliliruhusu kufanyika kwa kikao baina yake na Ludovick cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka Denis Msaki.

Washitakiwa wote hata hivyo walikanusha mashitaka hayo.

Hakimu Katemana akaamuru washitakiwa warejeshwe rmumande.


Source: http://www.wavuti.com/

No comments:

Post a Comment