Monday, April 1, 2013

LIONEL MESSI AVUNJA REKODI BARCELONA IKIBANWA UGENINI


Picha inayomuonesha mshambuliaji wa FC Barcelona ya Hispania, Lionel Messi, akiwa amezungushiwa logo za timu zote 19 za Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga,’ kuonesha tarehe za mechi na idadi ya mabao aliyoifunga kila timu ilipocheza na Barca msimu huu. (Picha zote kwa hisani ya gazeti la Daily Mail la Uingereza).
 Lionel Messi akichuana na mabeki wa timu ya Celta Vigo, wakati wa mechi ya La Liga iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
 Messi akichanja mbuga kumtoka mlinzi wa Celta Vigo wakati wa mechi baina ya klabu hizo jana Jumamosi.
 Mlinda mlango wa Celta Vigo, Javi Varas, akichumpa bila mafanikio kuokoa mchomo wa yoso Chriastian Tello kuiandikia Barca bao la kwanza.
 Lionel Messi akishangilia bao lake la kusawazisha lililomfanya avunje rekodi katika Ligi Kuu ya Hispania 'La Liga'

BARCELONA, Hispania

Messi amefunga bao ambalo licha ya kuipa Barca sare ya 2-2 dhidi ya Celta Vigo, lakini limemfanya kuwa nyota wa kwanza kufunga mabao kwa miezi mitano mfululizo, huku akiwa nyota wa pekee pia kuzichapa timu zote za ligi hiyo katika msimu mmoja

MSHAMBULIAJI Lionel Messi amezidi kuvunja rekodi za soka, baada ya jana Jumamosi kufunga bao lililomfanya aweke rekodi ya kufunga mabao katika kipindi cha miezi mitano mfululizo katika Ligi Kuu ya hapa La Liga.

Rekodi hiyo iko sambamba na ile ya kuwa nyota wa kwanza Hispania kufunga mabao katika kila mechi miongoni mwa klabu 19 za La Liga ukiondoa klabu yake ya FC Barcelona.

Mkali huyo anayeshikilia tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia kwa mwaka wa nne mfululizo, alifunga bao hilo kuipa Barcelona sare ya mabao 2-2 ugenini, ilipoifuata Celta Vigo, hivyo kumfanya afikishe mabao 43 kwa msimu huu.

Kwa bao la jana, Messi sasa amefunga jumla ya mabao 30 katika mechi 19 zilizopita, ambao ni wastani wa aina yake kwa mshambuliaji La Liga.

Ilikuwa ni Novemba 3 mwaka jana, wakati Messi alipoingia dimbani na kutoka bila kufunga bao, wakati Barca ilipoifuata Celta Vigo – mechi ambayo aliingia dimbani saa 24, tangu mpenzi wake Antonella Ruccuzzo, kumzalia mtoto wa kiume aitwaye Thiago.

Messi alihaha kwa dakika zote 90 za mtanange huo waliomaliza kwa kushinda mabao 3-1, lakini hakufanikiwa kupata bao la kumzawadia mtoto wake aliyezaliwa, lakini ametikisa nyavu kila mechi kuanzia usiku huo.

Kocha msaidizi wa FC Barcelona, Jordi Roura alimmwagia sifa mkali wake huyo na rekodi yake hii mpya, akisema: “Ukweli kwamba hakuna aliyewahi kufanya hivi hapo kabla, unathibitisha ugumu uliopo katika kuweka rekodi hii.”

Katika mtanange huo, Barcelona iliwapumzisha nyota wake kadhaa, jambo lililotafsiriwa kama kujiwinda na mechi ya kesho ya robo fainali mabingwa Ulaya dhidi ya PSG.

Daily Maily

No comments:

Post a Comment