Sunday, March 31, 2013

KUMBE ALIYEMUUA PADRE MUSHI ALIWAHI KUGOMBEA UBUNGE!!!!!!!!!

Picture
Mtuhumiwa (picha: FreeBongo blog)


IMEELEZWA kuwa, mtuhumiwa Omar Mussa Makame (35) anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kumuua Padri Evaristus Mushi ni mwanachama wa CUF ambaye aligombea nafasi ya uwakilishi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 katika Jimbo la Rahaleo kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF).

Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Hamad Masoud alithibitisha jana kuwa, mtuhumiwa huyo ni mwanachama wao na alishiriki katika mchakato wa uchaguzi mkuu na kusimamishwa na chama katika kampeni za Uwakilishi Jimbo la Rahaleo.

“Ni kweli mtuhumiwa anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya Padri Mushi ni mwanachama wetu na alishiriki katika mchakato wa kuwania Uwakilishi Jimbo la Rahaleo mwaka 2010.

Hata hivyo, Hamad alisisitiza na kusema suala la Omar kamwe lisihusishwe na CUF na kusema suala hilo watalitolea tamko baadaye.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ripoti ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Jimbo la Rahaleo, mgombea wa CCM, Nassor Salim Ali maarufu kama Jazirra aliibuka na ushindi kwa kupata kura 3,952 sawa na asilimia 63.10, wakati mgombea wa CUF, Omar Mussa Makame alipata kura 2,310 sawa na asilimia 39.9 na kushika nafasi ya pili.

Taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Jeshi la Polisi, Mussa Ali Mussa mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kukamatwa kwa Omar kunatokana na michoro ya teknolojia ya kisasa chini ya msaada wa upelelezi wa makachero kutoka FBI ambayo iliweza kutambua sura yake.

Uchunguzi zaidi uliofanywa na gazeti hili (HabariLeo) umegundua kwamba mtuhumiwa huyo licha ya kuwa mfuasi wa CUF, mama yake mzazi ni kada wa CCM. Mama yake, Tatu Sheha mkazi wa Mkele, Unguja ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi wa CCM katika Jimbo la Kwamtipura. Tangu kuibuka kwa kadhia hiyo inayomhusu mtoto wake, mama mzazi amekosa raha na faraja kiasi ya kushindwa kuhudhuria vikao vya chama kwa takribani wiki mbili sasa.

Baadhi ya wananchi Zanzibar wamepongeza juhudi za Jeshi la Polisi za kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, wakisema ni dalili njema za kutaka kukomesha matukio ya mauaji kisiwani Zanzibar.

Source: http://www.wavuti.com/

No comments:

Post a Comment