Saturday, February 16, 2013

YATIMA ABAKWA NA WATU KUMI, ASKARI NAYE BADALA YA KUMSAIDIA AKAMLAWITI

Picture
Nyumba inayoonekana ni ghorofa inayodaiwa kutumiwa kama danguro iliyopo Mwananyamala Magengeni jijini Dar es Salaam
Msichana yatima, mkazi wa mkoani Manyara, amefungiwa kwenye danguro  kwa zaidi ya miaka 10 akinyanyaswa kingono, kuteswa na kuambukizwa Virusi Vya UKIMWI  (VVU).

Msichana huyo aliyeondolewa nyumbani kwao Oysterbay mjini Babati,  alilaghaiwa na mwanamke aliyejifanya kuwa msamaria mwema, akitangaza  nia ya kumsaidia kielimu na kimaisha, kufuatia kifo cha mama yake mzazi.

Msichana aliyefikwa na masahibu hayo ni  Sara Tarimo (27) ambaye aliangukia mikononi mwa  mwanamke mwenye danguro hilo, Abia Lucas (44) anayeishi Mwananyamala Magengeni. Ilikuwa ni baada ya kifo cha mama yake  Magreth Kitinati, aliyekuwa akiishi naye  Oysterbay huko Manyara.

Sara anasema mwanamke huyo alimtoa kijijini kwao hadi jijini Dar es Salaam, na kumshinikiza kwenye ‘utumwa wa ngono’ kwa kipindi cha miaka 10 akiwa amefungiwa ndani.

Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, mama yake mzazi alifariki, hivyo ujio wa msamaria huyo ulikuwa faraja na tumaini jipya kwa maisha yake. Haikuwa hivyo. Sara alisema  alipoteza bikra yake baada ya kumlazimisha kufanya ngono  na mwanamume mtu mzima, aliyembaka na ukawa mwanzo wa kutumiwa kingoni na wanaume wa kila aina.

Sara alisema alifanywa unyanyasaji huo akiwa na miaka 13 na kwamba hilo lilikuwa   tukio lake la kwanza kukutana na mwanaume. Baada ya kufanikiwa kutoroka na kuwataarifu polisi nyendo za mama huyo ambaye sasa anashikiliwa kwa mahojiano, Sara anasimulia kumbukumbu za kusikitisha za miaka aliyoipoteza katika himaya ya danguro la ‘msamaria.’

HISTORIA YAKE 

Sara ni mmoja wa watoto watatu katika familia yao. Kaka  yake  Emmanuel Tarimo (31) na dada yake Neema Tarimo.

Wakati akipochukuliwa na ‘msamaria’ alimuacha kaka yake huko Babati akijitafutia riziki kwa kubeba mizigo na dada yake akiendelea na masomo ya shule ya msingi. Anasikitika kuwa katika maisha yake hakubahatika kumfahamu baba yake, lakini aliwahi kuelezwa na mama yake kuwa ni mwenyeji wa Kilimanjaro.

Mama yake ndiye aliyekuwa anatunza familia yao licha ya  kwamba hakuwa na ajira rasmi, wala biashara za kudumu. Mazingira hayo, yalimlazimisha kukatisha masomo  akiwa darasa la tatu katika shule ya Msingi Idangunyii. Anasema alikuwa na ndoto ya kupata elimu zaidi, lakini kifo cha mama yake kilisababisha ajione kuwa  hana bahati. 

Source: NIPASHE

No comments:

Post a Comment